Cabo Delgado!

20 Januari 2021

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu na kuongezeka kwa ghasia katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji.
 

Wakurugenzi wa kikanda wa Umoja wa Mataifa kwa ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika wameelezea wasiwasi wao huo hii leo kupitia taarifa yao ya pamoja iliyotolewa mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Wameema ghasia zinazoendelea zimefurusha maelfu ya watu makwao na kutegemea zaidi misaada ya kibinadamu.
“Kwa mujibu wa serikali ya Msumbiji, vikundi vilivyojihami vimefanya mashambulizi na kulazimu watu zaidi ya 565,000 kukimbia vijiji vyao na kuacha mazao shambani na vyanzo vyao vya kujipatia kipato,”  imesema taarifa hiyo.

Mwezi uliopita wa Desemba, wakurugenzi hao walitembelea Msumbiji kutathmini hali halisi na mahitaji ya wakazi wa eneo hilo na jamii zinazowahifadhi huko Cabo Delgado na pia kukutana na maafisa wa serikali. 
Katika ziara hiyo, wiongozi hao waandamizi walitoka mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la chakula na kilimo, FAO, idadi ya watu UNFPA, maendeleo ya kilimo IFAD, uhamiaji IOM, kuhudumia wakimbizi UNHCR, mpango wa chakula duniani, WFP na maendeleo UNDP pamoja na viongozi kutoka ofisi ya Umoja wa Mataifa Msumbiji.

Wakimbizi wa ndani jimboni Cabo Delgado wakisubiri msaada wa chakula kutoka shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP kwenye wilaya ya Metuge jimboni Cabo Delgado.
WFP/Falume Bachir
Wakimbizi wa ndani jimboni Cabo Delgado wakisubiri msaada wa chakula kutoka shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP kwenye wilaya ya Metuge jimboni Cabo Delgado.

Walieleza hofu yao kubwa juu ya kuendelea kuibuka kwa janga la kibinadamu ambako wananchi wanakumbwa pia na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na pia wanakosa huduma muhimu ikiwemo chakula.
Hali ya usalama inavyozidi kudorora na miundombinu kuzidi kuharibika inamaanisha inakuwa vigumu kufikia wananchi na janga la COVID-19 limefanya hali kuwa mbaya zaidi.

Sauti za manusura Cabo Delgado

Wakazi wa maeneo ya Ancuabe na Chiúre  jimboni Cabo Delgado wakiwemo wanawake, wanaume na watoto walifunguka kuhusu kile kinachowakumba ikiwemo ukosefu wa usalama na kushindwa kufanya shughuli za kujipatia kipato.

Pamoja na kutambua kuwa hatua kadhaa zimechukuliwa kusaidia jamii hizo, viongozi hao wamesisitiza kuwa kutokana na idadi ya wakimbizi kuendelea kuongezeka kila uchao, ukosefu wa maji safi na salama, chakula, malazi, afya na elimu unazidi kufanya hali kuwa mbaya zaidi kuwa hata awali mahitaji hayo hayakuwa yanatosheleza.

Wakati msimu mwingine wa mvua unatarajiwa hivi karibuni, viongozi hao wamesema madhara ya vimbunga Idai na Kenneth ni kumbusho kuwa eneo hilo liko hatarini tena kupigwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Janga la Corona nalo limesababisha shule kuendelea kufungwa, na hivyo viongozi hao wametilia shaka uwezekano wa uwekezaji wa dhati wa kijamii kwenye elimu na nguvu kazi.

Kinachohitajika sasa

Taarifa hiyo ya pamoja inataka hatua za dharura za ulinzi kwa jamii hizo sambamba na huduma muhimu kama vile chakula, afya, lishe bora kwa watoto na wanawake walioko hatarini pamoja na chanjo na huduma za ushauri nasaha na kupatia uwezo wakimbizi wavuvi na wakulima kuweza kurejea katika shughuli zao za kujipatia kipato.
Wakurugenzi hao wa kikanda wa Umoja wa Mataifa wamesisitiza umuhimu wa kuunga mkono vya kutosha kupatia makazi mapya familia zilizofurushwa makwao.

Kuhusu mbinu za kudhibiti misimamo mikali, wakurugenzi hao wametoa wito kwa kuanzishwa kwa mipango mipya ya kupatia kipaumbele uwezeshaji kiuchumi jamii na ujumuishwaji wa kijamii na kisiasa kwa vijana na wanawake.

Wameisihi serikali ya Msumbiji na jamii ya kimataifa kuimarisha juhudi za kumaliza aina zote za ukatili nchini humo ikiwemo ukatili wa kijinsia na ndoa katika umri mdogo na kuwekeza zaidi kwa wasichana na wanawake kwa kuwa wao ndio mawakala wa maendeleo.

Wametamatisha taarifa yao kwa kushukuru serikali ya Msumbiji kwa dhima yake katika kusaidia kukidhi mahitaji ya kibinadmu kwa wakazi wa kaskazini mwa nchi hiyo na kusisitiza azma ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia haki za binadamu na kuendeleza amani na maendeleo endelevu kwa wakazi wote wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter