Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaendelea kutiwa hofu na Tanzania kurejesha kwa nguvu wakimbizi wa Msumbiji:UNHCR

Mgogoro katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji umesababisha janga la kibinadamu.
© WFP/Shelley Thakral
Mgogoro katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji umesababisha janga la kibinadamu.

Tunaendelea kutiwa hofu na Tanzania kurejesha kwa nguvu wakimbizi wa Msumbiji:UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limesema linaendelea kutiwa hofu na taarifa za kulazimishwa kurejea nyumbani kwa familia kutoka Msumbiji zilizokimbilia Tanzania.  

Shirika hilo limetoa wito kwa nchi jirani na Msumbiji kuendelea kuheshimu sheria ya kuwapa fursa watu wanaoomba hifadhi kwa sababu wanakimbia machafuko na vita Kaskazini mwa Msumbiji. 

UNHCR imesema hadi kufikia Mei 28 mwaka huu watu wapatao 62,001kutoka eneo la Palma walitawanywa kwa sababu ya mashambulizi kutoka makundi ya wapiganaji yasiyo ya kiserikali (NSAGs) tangu mwezi Machi. 

Shirika hilo limesema familia zimeendelea kuvuka mpka na kukimbia hali tete ya usalama hasa katika maeneo ya Mueda, Nangade, Montepuez na Pemba na wanakimbia kwa kutumia usafiri wa ardhini, ang ana baharini. 

Kabla ya mashambulizi ya Palma, watu takriban 700,000 tayari walikuwa wametawanywa katika majimbo ya Cabodelgado, Nampula, Niassa, Sofala na Zambezia kutokana na machafuko na usalama mdogo jimboni Cabo Delgado. 

Hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota na msaada wa haraka unahitajika ili kushughulikia mahitaji ya watu wanaokimbia machafuko limesisitiza shirika hilo.