Skip to main content

Watu 350,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu Goma DRC:UNHCR 

Watoto wako hatarini kufuatia kulipuka kwa volkano Goma nchini DRC.
© UNICEF/Olivia Acland
Watoto wako hatarini kufuatia kulipuka kwa volkano Goma nchini DRC.

Watu 350,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu Goma DRC:UNHCR 

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema msaada wa haraka wa kibinadamu unahitajika kuwasaidia maelfu ya watu walioathirika na mlipuko wa volcano iliyolipuka tarehe 22 Mei mwaka huu kwenye mlima Nyiragongo mjini Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. 

Kwa mujibu wa makadirio ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR watu 350,000 wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu kwani watu 450,000 wameukimbia mji wa Goma na 120, 000 miongoni mwao wamewasili kwenye mji wa Sake katika jimbo la Kivu Kaskazini. 

Waliokimbia waanza kurejea 

UNHCR inasema wengi wa watu 8,000 ambao walikuwa wamevuka mpaka kuingia nchi Jirani ya Rwanda wameanza kujerea.  

Watu hao waliokimbia makazi yao walikuwa wakilindwa na familia zilizowakaribisha, wakati wengine walikuwa wakikaa katika makanisa na shule zilizojaa watu wengi.  

Watu waliohamishwa walikuwa na mahitaji ya haraka ya nyumba na vitu vya msingi, na hawakuweza kurudi makwao kufuatia agizo la kuwahamisha kwenye vitongoji vinane vya Goma ambavyo vilikuwa katika hatari zaidi ya mlipuko mwingine. 

 Mara tu baada ya kufika Sake, UNHCR ilikuwa imeanza kusaidia watu ambao walikuwa wameondoka Goma walifuata agizo la uokoaji.  

Tangu Mei 28, shirika hilo limekuwa likitoa makazi ya jamii kwenye shule na makanisa, na msaada wa vitu vya msingi ikiwemo maturubai, blanketi na vifaa vya usafi.  

Msaada huo ulikuwa umetolewa kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za jamii ya kimataifa, lakini hautoshi kukidhimahitaji yote. Tathmini iliyofanyika katika mji wa Goma inaonyesha kwamba malazi, chakula na maji vinahitajika haraka. 

UNHCR sasa inajikita kujenga eneo maalum ambalo litawaruhusu watu waliohamishwa kuondoka shuleni na makanisani na kuishi hapo, na pia kuwaruhusu watoto kurudi darasani.  

Shirika hilo pia limetuma timu kwenda Rutshuru, kilomita 70 Kaskazini Mashariki mwa Goma, kusaidia juhudi huko na kuungana na idadi kubwa ya wakimbizi ambao tayari walikuwa katika eneo hilo 

 UNHCR tayari ilikuwa inakabiliwa na changamoto kubwajimboni Kivu Kaskazini kabla ya zahma hii ya hivi karibuni, kwani mizozo na vurugu zilikuwa zimetawanya watu zaidi ya milioni 2 katika jimbo hilo, wakiwemo  450,000 mwaka huu wa 2021 pekee.