Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashauriano ya kisiasa ndio suluhu ya mzozo kati ya Palestina na Israel- Guterres

Baraza la Usalama la UN likiwa kwenye kikao kwa njia ya mtandao jumapili Mei 16, 2021 kujadili Mashariki ya Kati na suala la Palestina
Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la UN likiwa kwenye kikao kwa njia ya mtandao jumapili Mei 16, 2021 kujadili Mashariki ya Kati na suala la Palestina

Mashauriano ya kisiasa ndio suluhu ya mzozo kati ya Palestina na Israel- Guterres

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao cha dharura kuhusu mapigano yanayoendelea kati ya waisrael na wapalestina huko Mashariki ya Kati ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mwelekeo pekee wa kutatua mvutano kati ya pande mbili hizo ni mashauriano ya kuwezesha kuwepo kwa mataifa mawili yaani Palestina na Israel.

UN Chief: Bloodshed must stop immediately

 

Akihutubia kikao hicho kilichoitishwa na China ambayo inashikilia urais kwa mwezi huu wa Mei, Bwana Guterres amesema kuwepo kwa mataifa mawili katika mazingira ya amani yakitambua kuwa Yerusalem ndio mji mkuu wa pande zote hizo ndio njia pekee ya kumaliza kinachoendelea sasa.

“Kadri mzunguko wa ghasia unavyoendelea, ndivyo hali inazidi kuwa ngumu kufikia lengo hilo la kuwa na mataifa mawili. Suluhu la kisiasa ndio litamaliza kabisa mzunguko wa ghasia na kuwezesha mustakabali salama na wenye amani kwa wapalestina na waisrael,” amesema Guterres.

Akizungumzia madhila yanayotokana na mapigano, Katibu Mkuu amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na mashambulizi yanayotoka pande zote, yaani Israel na Palestina akisema, “nchini Israel, ghasia kutoka kwa makundi ya kibabe zinaongeza upana zaidi wa janga. Nina wasiwasi mkubwa pia na mapigano kati ya vikosi vya ulinzi vya Israel na wapalestina kwenye eneo la wapalestina linalokaliwa huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ikiwemo Yerusalem Mashariki ambako baadhi ya familia za kipalestina ziko hatarini kufurushwa. Viongozi wa pande zote wana wajibu wa kudhibiti kauli za chuki na kuleta utulivu wakati huu ambapo mvutano unazidi kuongezeka.”
Maelfu ya wapalestina wamefurushwa makwao huko Gaza na sasa wamesaka hifadhi kwenye shule, misikiti na kwingineko wakiwa hawana huduma za msingi kama vile maji na afya huku hospitali zikiwa zimezidiwa uwezo kutokana n ajanga la COVID-19.

Na huko huko Israel nako raia wanaishi kwa hofu kutokana na mashambulizi ya maroketi kutoka Gaza.

Katibu Mkuu pia ameeleza masikitiko yake kufuatia shambulio dhidi ya kambi ya wakimbizi huko Gaza ambako watu 10 wa familia moja waliuawa akisema maeneo ya aina hiyo lazima yalindwe.

Amegusia pia shambulio dhidi ya jengo la vyombo vya habari huko Gaza akisema wanahabari nao lazima waruhusiwe kufanya kazi zao kwa uhuru bila uoga au manyanyaso.

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kutekeleza jukumu lake kwa kushirikiana na Palestina na Israel na wadau wa kimataifa na kikanda ikiwemo pande nne za kumaliza mzozo Mashariki ya Kati ili kupata amani ya kudumu.

Mapigano ya sasa huko Gaza yameanza tarehe 10 mwezi huu wa Mei.