Skip to main content

Hatutaki tena kuzurura mitaani, tunachapa kazi: Vijana Itigi, Singida 

Simon Philipo Sirilo, mnufaika wa miradi ya Restless Development nchini Tanzania.
Restless Development Tanzania
Simon Philipo Sirilo, mnufaika wa miradi ya Restless Development nchini Tanzania.

Hatutaki tena kuzurura mitaani, tunachapa kazi: Vijana Itigi, Singida 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania vijana katika wilaya ya Itigi mkoani Singida wameshika hatamu ya maisha yao kwa kuamua kuachana na kukaa “vijiweni” na badala yake kushiriki katika ujasiriamali na hivyo kwenda sambamba na wito wa Umoja wa Mataifa wa kuondokana na umaskini. 

Miongoni mwao ni Waziri Boniface yeye anasema “kutoka kuwa mtu wa mtaani hadi kijana mwajiriwa katika kiwanda cha kutengeneza chaki na mikanda itokanayo na jasi.” 

Bwana Waziri anasema, “nilikuwa sina kazi, niko mtaani, kwa hiyo nikashukuru Mungu nimeajiriwa kiwanda hiki hapa cha Mloa. Najishughulisha na kazi za kiwandani. Kwa hiyo napenda kuwashauri vijana wenzangu wanaokaa mtaani ambao hawatafuti kazi, kazi za kuzungukazunguka  mtaani si nzuri. Nafanya kazi ya kutengeneza unga wa chaki na mikanda, nasagisha na kuchoma unga wa chaki na mikanda na sasa hivi nina muda wa miaka mitatu.” 

Soundcloud

 

Lakini nini chanzo cha mafanikio haya ya Bwana Boniface ya kutoka mtaani hadi kiwandani? Leonard Gelila katibu wa Umoja ambamo Boniface anafanya kazi, anafafanua akisema, “Tuna Umoja wetu ambao ni kikundi tuliosajli mwaka jana baada ya kuwepo na changamoto nyingi zilizotokana na mtu kufanya kazi peke yake. Soko lilikuwa ni shida na zaidi ya yote ubora. Hatukwa na ubora unaofanana, kila mtu alitengeneza hii poda kwa ubora wake. Kwa hiyo sokoni kukawa na shina. Kuna ambao ubora ulikuwa juu na wengine chini, kwa hiyo poda kutoka Itigi ikaonekana haina ubora.  Kwa hiyo tukawa na Umoja ambao kimsingi ni kuwa na ubora unaofanana na pia kumaliza tatizo la soko.  

Tukamuuliza Bwana Gelila je Umoja umekuwa na mafanikio yoyote? 

“Tangu tuwe na huu umoja imekuwa ni msaada mkubwa kwa maana sasa poda yetu imekuwa bora  kutokana na kamati zetu mbili, ambapo kuna kamati ya kusimamia ubora kuanzia uandaaji hadi kukamilika, na pia kamati ya kufuatilia soko pekee. Sasa hivi naona faida ya Umoja na tutaenda mbele zaidi. Hadi sasa tuna vijana zaidi ya 42 ambao tunafanya nao kazi, kama vibarua ambao imewapunguzia ukali wa maisha. Awali ilikuwa sivyo, walikuwa wanakaa tu vijiweni. Kuna wa kike na wa kiume. Kwa hiyo kuna manufaa katika ujasiriamali ambao awali tuliwaza kuajiriwa lakini sasa tangu nijihusishe katika biashara hii sina tamaa ya kuajiriwa.” 

Tweet URL

Nusra ni miongoni mwa wafanyakazi wanawake katika kiwanda hiki kinachotengeneza mikanda ya kupamba kwenye dari na kuta za nyumba, mikanda yenye maua ya aina mbalimbali ya kupendeza. Kazi hii ni nadra kufanywa na wanawake.  Nusra akielezea jukumu lake anasema, ““Najishughulisha kuchakata pamoja na kuosha, na pia tunajishughulisha kutengeneza mikanda, kama unavyoiona. Nawashauri wanawake wenzangu, hii ni kazi ambayo inatupatia fedha, na kukuza ajira, hivyo nashauri wanawake wenzangu kujishughulisha ili tufikie malengo.” 

Simon Sirilo, muasisi wa kiwanda hiki anasema hawajapata msaada popote. Mtaji unatokana na kila mwanaumoja,  ambapo yeye binafsi alidunduliza mshahara wake hadi kuweza kufanikisha lengo la kuwa na kiwanda, kiwanda ambacho eneo lake wamekodisha. Lakini mchakato mzima hadi kutengeneza bidhaa unakuwa vipi? 

“Utengenezaji wa unga wa gypsum au jasi, una mchakato wake. Tunaanza mbugani ambako  kuna watu wanatuchimbia mawe, tukishanunua kuna vijana tuliowaajiri ambao wanaosha hayo mawe, baadaye vijana wengine wanachoma yale mawe, tukishachoma tunausagisha na tunapata unga wa kutengeneza chaki pamoja na mikanda.” 

Bwana Sirilo akaenda mbali zaidi kuhusu walichokifanikisha akisema, “Kupitia Gypsum hii tumeweza kujiajiri na pia kuajiri vijana wengine. Na hivyo vijana wameweza kujikwamua kiuchumi, tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wanahangaika. Rai yangu kwa vijana wote walioko Itigi wajishughulishe katika mambo ya kujiinua kiuchumi na pia waje hapa tuungane kutengeneza mikanda na chaki. Kupitia hapa tunaamini kuwa vijana watajiinua kiuchumi na tunakaribisha wengine walioko ndani na nje ya nchi watutembelee ili waweze kuona vijana tunachotengeneza na kisha tunaweza kupanua wigo wa masoko siyo tu Tanzania bali hata nje ya Tanzania.”