Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uelewa wa usawa wa jinsia wabadili maisha ya kaya Ruvuma nchini Tanzania

Wafanyabiashara wanawake Tanzania wamesaidia kukuza kiwango cha uchumi kutokana na harakati zinazoendelea za usawa kijinsia.
Picha na UNCTAD
Wafanyabiashara wanawake Tanzania wamesaidia kukuza kiwango cha uchumi kutokana na harakati zinazoendelea za usawa kijinsia.

Uelewa wa usawa wa jinsia wabadili maisha ya kaya Ruvuma nchini Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ainisho la suala la usawa wa kijinsia limekuwa likileta utata hasa pale ambapo jamii haijaweza kushirikishwa vyema kutambua manufaa ya suala hilo. Huko wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma nchini Tanzania,  suala hilo ambalo ni lengo namba tano la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs sasa limeanza kushika kasi.

Mradi wa Timiza Ahadi unaotekelezwa na shirika la kiraia la Restless Development katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma nchini Tanzania umeleta mabadiliko makubwa hasa katika uelewa wa usawa wa kijinsia na kuinua vipato hususan vya kaya.

Akihojiwa na Idhaa hii jijini New York, Marekani kando mwa jukwaa la ngazi ya juu linalotathmini utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, mchechemuzi wa vijana kupitia shirika hilo Judith Kitinga amesema wameweza kuelimisha jamii kuhusu maana ya usawa wa kijinsia. 

Usawa wa kijinsia si kwamba mwanaume avae sketi, la hasha

Amesema kuwa "usawa wa kijinsia si kwamba mwanaume avae sketi, la hasha," bali ni kuwepo kwa mfumo ambamo kwao wanaume na wanawake wanashirikiana katika utekelezaji wa majukumu ya familia na pia kuondokana na mifumo dume ambayo inaleta shari zaidi kwa familia. 

Bi. Kitinga ambaye anafanya kazi hiyo kwa kujitolea akatoa mfano wa mabadiliko waliyoshuhudia tangu kuanza kwa mradi huo miezi minne iliyopita. akimtaja mwanamke mmoja ambaye mume wake baada ya kuelewa maana ya usawa wa kijinsia sasa amempatia hata mtaji wa biashara na maisha yao yamekuwa bora zaidi.

Mradi huo unatekelezwa katika mikoa mitatu ya Tanzania ambayo ni Dodoma, Iringa na Ruvuma.