Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia mpya jimboni Ituri DRC zaweka watoto katika hali mbaya zaidi- UNICEF

Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Drodro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC
© UNICEF/Roger LeMoyne
Watoto wakimbizi wa ndani wakicheza katika kituo rafiki kwa watoto kambini Drodro, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC

Ghasia mpya jimboni Ituri DRC zaweka watoto katika hali mbaya zaidi- UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, limesema mapigano yaliyoanza tena hivi karibuni katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, yanazidi kuhatarisha hatma ya watoto sambamba na ripoti za ukiukwaji wa haki za wanawake.
 

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo mjini Kinshasa, DRC imesema ongezeko hilo la madhila linakuja licha ya wito wa mara kwa mara wa UNICEF na mashirika ya kibinadamu ya kuonya dhidi ya ghasia hizo ambazo ni pamoja na watu kukatwa na mapanga na ukatili wa kingono.
Kwa mujibu wa UNICEF, tangu mwezi Januari mwaka hu uhadi sasa kumekuwepo na matukio 175 ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwemo watoto kutumikishwa kwenye vikundi vilivyojihami kijeshi, watoto kuuawa na wengine kukatwa viungo, ukatili wa kingono na mashambulizi dhidi ya shule na hospitali.

Katika maeneo yenye matukio mengi, wafanyakazi wa kibinadamu walizuia kufika kwenye maeneo hayo hususan yale ya Djugu na Irumu.

Idadi kubwa ya watu wamefurushwa makwao kutokana na mashambulizi yanayoendelea, ambapo watoto zaidi ya 275 miongoni mwao wasichana 118 wamepotezana na wazazi wao jimboni Ituri.

“Tunaendelea kupaza sauti kuhusu hali mbaya ya watoto jimboni Ituri, kwa sababu hatutaki dunia isalie na ganzi dhidi ya janga hili la kibinadamu,” amesema Jean Metenier, Mratibu mwandamizi wa UNICEF mashariki mwa DRC.

Amesema kila siku watoto na haki zao vinasiginjwa kupitia ghasia zisizo na ukomo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, kufurushwa, ukosefu wa chakula na kushindwa kupata huduma za msingi ikiwemo kujisomea.

“Tunasema tena na tena; tunahitaji jamii ya kimataifa iongeze juhudi kwa kuwa operesheni zetu bado hazijadikidhi kile kiwango ambacho tunatakiwa,” amesema mratibu huyo mwandamizi wa UNICEF Mashariki mwa DRC.

Zaidi ya watu milioni 1.6 wanakadiriwa kuwa wakimbizi wa ndani jimboni ITuri, kati ya watu milioni 5.7 wakazi wa jimbo hilo.

Anwarita akiwa nyumbani kwa wazazi wake walezi huko Bona, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
© UNICEF/Roger LeMoyne
Anwarita akiwa nyumbani kwa wazazi wake walezi huko Bona, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Na sasa watu milioni 2.8 kati yao hao wanahitaji msaada  wa dharura.

Hali ya Watoto Ituri

Takwimu za karibuni zaidi zinaonesha kuwa zaidi ya watoto 100,000 jimboni Ituri wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo uliokithiri, ikiwa ni matokeo ya moja kw amoja ya ukosefu wa chakula ambao unakumba watu wapatao 800,000.

Mashambulizi ya shule yamesababisha wakimbizi wa ndani 400,000 na watoto waliorejea wenye umri wa kati ya miaka 6-11 kutokwenda shuleni kwenye miji ya Djugu, Irumu na Mahagi;

Na zaidi ya hapo ni mtu mmoja tu kati ya watatu jimboni Ituri ana huduma za kujisafi.