Mashambulizi dhidi ya raia yaongezeka Beni: UNHCR
Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema lina wasiwasi kuhusu usalama wa maelfu ya raia katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, DRC ambako ghasia za makundi yenye silaha zimeongezeka na za hivi karibuni zimesababisha vifo vya watu zaidi ya 20. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.
Wasiwasi huo wa UNHCR umeelezwa leo na msemaji wa shirika hilo, huko Geneva, Uswisi, Babar Baloch wakati akizungumza na waandishi habari kuelezea hali ilivyo wakati huu ambapo kuna kampeni ya kutokomeza mlipuko wa Ebola.
Bwana Baloch amesema mashambulio yanaongezeka katika mji wa Beni ulioko jimbo la Kivu Kaskazini pamoja na jimbo la Ituri, maeneo ambayo yako mpakani mwa DRC na Uganda.
Amesema mwishoni mwa wiki kundi la ADF- NALU lilishambulia Beni na kuua watu zaidi ya 20 wengi wao raia na kwamba , "“Hii ni mara ya kwanza mapigano kufika katika mji wa Beni. Na katika shambulio lingine katika mji wa Oicha, karibu na Beni kundi lililojihami ambalo linashukiwa kuwa la ADF-Nalu, lilimuua kwa kumpiga risasi, mtu mmoja mwenye umri wa miaka 47 na kuteka takribani watoto wanane, walipora mali na kisha kuzichoma moto nyumba kadhaa .”
Kwa mantiki hiyo amesema UNHCR inatoa wito kwa wanaohusika katika mgogoro huo kuheshimu na kulinda maisha ya watu waliopoteza makazi yao katika eneo hilo ambalo tayari linakabiliwa na mlipuko wa Ebola.
Kuhusu watu wanaovuka mpaka hadi Uganda wakikimbia ghasia kutoka DRC, UNHCR inasema kuwa idadi bado ni ile ile ambapo kwa wastani kwa siku wakimbizi 200 huingia Uganda na kwa mwezi ni 600.
Hata hivyo amesema, “Kuwasili kwa wakimbizi ni sehemu ndogo tu ya mwelekeo wa kila siku wa watu wanaovuka mpaka wa DRC na Uganda kwa sababu zingine kama vile biashara au kutembelea jamaa na marafiki na masuala mengine.”
Amesema ili kuepusha kuenea kwa Ebola, UNHCR inachangia juhudi za shirika la afya duniani WHO pamoja na serikali ya Uganda kuwapima watu wanaovuka mpaka hadi Uganda na imeweka vituo kadhaa vya kuwapimia kiafya wakimbizi na hadi sasa hakuna kisa chochote cha Ebola kilichoripotiwa kutoka kwa wakimbizi.