Skip to main content

Moto waua wagonjwa 82 hospitalini Iraq, UN yataka hatua zaidi za ulinzi

Kuta katika eneo la Shualah kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad ukiwa na picha za kuelimisha familia jinsi ya kupatia matibabu mgonjwa wa COVID-19 pindi wanapokuwa nyumbani
UNAMA
Kuta katika eneo la Shualah kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad ukiwa na picha za kuelimisha familia jinsi ya kupatia matibabu mgonjwa wa COVID-19 pindi wanapokuwa nyumbani

Moto waua wagonjwa 82 hospitalini Iraq, UN yataka hatua zaidi za ulinzi

Afya

Umoja wa Mataifa umeelezea mshtuko wake na machungu makubwa kufuatia vifo vya watu 82 vilivyotokea baada ya moto mkubwa kulipuka katika hospitai ya Ibn Khatib inayotibu wagonjwa wa COVID-19 kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Hospitali hiyo  iliwaka moto usiku wa Jumamosi ambapo zaidi ya watu 100 wameripotiwa kujeruhiwa, vyombo vya Habari vikidai kuwa chanzo cha moto ni mlipuko wa mtungi wa hewa ya oksijeni.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq,  Jeanine Hennis-Plasschaert, ametumia taarifa iliyotolewa leo mjini Baghad kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza Maisha huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

UN yataka uchunguzi

Mwakilishi huyo ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq, UNAMI, metoa wito kwa mamlaka kuchukua hatua thabiti kuhakikisha janga kama hilo halitokei tena.

Kwa mujibu wa vyombo vya Habari, Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi amemsimamisha kazi Waziri wa afya na kuagiza uchunguzi wa tukio hilo ufanyike haraka.

Halikadhalika amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kutoa msaada muhimu kwa sekta ya afya nchini Iraq wakati huu ambapo janga la Corona linazidi kushika kasi nchini humu, akiongeza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kutoa msaada zaidi na kusaidia mamlaka za afya kudhibiti ugonjwa huo.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kupitia mtandao wa Twitter limetuma salamu za rambirambi huku likitakia ahueni majeruhi.

Hali ya COVID-19 Iraq

Nchini Iraq, ugonjwa wa Corona umekuwa mzigo mkubwa kwa mfumo wa afya ambapo hospitali zimezidiwa uwezo na takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, tangu mwezi Januari mwaka jana 2020 hadi sasa, Iraq imekuwa na wagonjwa zaidi ya milioni 1 wa Corona ambapo kati yao hao 15,217 wamefariki dunia. Halikadhalika takwimu zinaonesha ongezeko la maambukizi tangu mwezi Februari mwaka huu.

Mwezi uliopitam Iraq ilizindua kampeni ya chanjo dhidi ya Corona baada ya kupokea shehena ya kwanza ya chanjo za COVID-19 kupitia mfumo wa COVAX, unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa chini ya uratibu wa pamoja wa WHO, ushirika dhidi ya magonjwa ya milipuko, CEPI na fuko la chanjo duniani, GAVI.