Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanafunzi wakimbizi Iraq wanufaika na ubunifu wa Mwalimu wakati wa COVID-19  

Ibrahim Yousef, mwalimu wa kemia anayefundisha kwa njia ya mtandao.
UNHCR/Firas Alkhateeb
Ibrahim Yousef, mwalimu wa kemia anayefundisha kwa njia ya mtandao.

Wanafunzi wakimbizi Iraq wanufaika na ubunifu wa Mwalimu wakati wa COVID-19  

Utamaduni na Elimu

Mwalimu mmoja nchni Iraq baada ya kuona shule nchini humo zimefungwa kutokana ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, aliamua kutumia mitandao ya kijamii kuwafundisha wanafunzi, hususani somo la kemia na wanafunzi wanasema mbinu hiyo imewasaidia mno.

Kama ilivyo katika maeneo mengine duniani, Iraq nako shule zilifungwa ili kupambana na ugonjwa wa coronavirus">COVID-19 na kuongeza changamoto hususani kwa wanafunzi wakimbizi. 

Mwalimu Ibrahim alitaka kutafuta njia ya kuwasaidia wanafunzi wa sekondari kusoma na kufaulu mitihani ya kemia katika mazingira hayo ambayo wasingeweza kufika shuleni. Ndipo akaanzisha chaneli yake ya Youtube ambayo anaitumia kufundisha hususani wanafanzi wakimbizi.  

Anachofanya Mwalimu Ibrahim ni anaweka simu yake mbele ya ubao wa kufundishia, kisha anatoa maelezo ya somo husika huku simu ikirekodi video hiyo ambayo anaiweka katika mtandao wa Youtube. 

Mwalimu Ibrahim pia ameanzisha makundi kwenye mitandao ya kijamii na anawaruhusu wanafunzi kumuuliza maswali ya moja kwa moja, na mara zote anawajibu. Mwalimu Ibrahim anasema, “Niliweza kumaliza mtaala mzima chini ya miezi miwili. Ninaendelea kuwasiliana na wanafunzi wangu. Nina vikundi kwenye WhatsApp na Viber. Wakati mwingine baada ya saa sita usiku wananitumia maswali na ninawajibu.” 

Yafa ambaye ni mwanafunzi anayesoma kwa njia hiyo ya mtandao, anaonekana akiangalia maelekezo ya Mwalimu Ibrahim kupitia mtandao wa Youtube, analinganisha kwenye kitabu na kisha anaandika katika daftari lake. Yafa anaelezea namna ambavyo mbinu ya Mwalimu Ibrahim imemsaidia,  "Ni vigumu kuelewa kila kitu wakati inapobidi kujisomea wewe mwenyewe. Mwalimu anahitaji kuelezea masomo. Nilisoma vizuri na kupata asilimia 86 katika kemia.”