Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN, AU, EU na IGAD watoa ushauri wa pamoja kwa Somalia

Watoto wakiwa wamesimama mbele ya Kanisa la Mogadishu lililojengwa na mamlaka za kikoloni za waitaliano nchini Somalia. (Maktaba)
IRIN/Kate Holt
Watoto wakiwa wamesimama mbele ya Kanisa la Mogadishu lililojengwa na mamlaka za kikoloni za waitaliano nchini Somalia. (Maktaba)

UN, AU, EU na IGAD watoa ushauri wa pamoja kwa Somalia

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika, Muungano wa Ulaya EU na Mamlaka ya pamoja ya kiserikali kuhusu maendeleo, IGAD, kupitia mkutano waliofanya kwa njia ya mtandao, wametoa tamko la pamoja kutokana na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Somalia.  

Mkutano huo uliofanyika juzi Ijumaa uliitishwa kwa kuzingatia uzito wa mkwamo wa kisiasa unaoendelea nchini Somalia kuhusu kufanyika kwa uchaguzi uliocheleweshwa, na mkwamo unaoendelea katika mazungumzo kati ya Serikali ya Shirikisho na baadhi ya viongozi wengine wa majimbo wanachama wa shirikisho. 

Kufuatia mazungumzo haya, AU, EU, IGAD na UN, wamesisitiza heshima yao kwa taifa hilo, uadilifu wa eneo, uhuru wa kisiasa na umoja wa Somalia; na kutoa wito kwa viongozi wa Somalia kutanguliza masilahi ya kitaifa ya Somalia na kurudi mara moja kwenye mazungumzo kutafuta suluhu juu ya masuala yaliyosalia, na kuhakikisha kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa ambazo zinaweza kudhoofisha utulivu wa Somalia, ambayo ni muhimu kwa kudumisha amani ya kimataifa na usalama. 

Wametia mkazo kwamba, "mkataba wa Septemba 17 unabaki kuwa njia inayofaa zaidi kuelekea uchaguzi, na wakawasihi Serikali ya Shirikisho na viongozi wa nchi Wanachama wa Shirikisho kupitia na kuthibitisha mapendekezo ya Kamati ya Ufundi ya Baidoa ya 16 Februari 2021 na kutafuta makubaliano kwa njia ya maelewano juu ya masuala yoyote muhimu kwa utekelezaji wa haraka wa uchaguzi." 

Aidha wametambua juhudi za wadau wa Kimataifa katika kuwezesha mawasiliano kati ya viongozi wa Somalia; na kutoa wito kwa Washirika kuimarisha mazungumzo haya mazuri na kutambua ikiwa inahitajika.  

Pia wameonesha wasiwasi mkubwa kwamba mkwamo wa kisiasa unaathiri vibaya amani, usalama, utulivu, na ustawi nchini Somalia na kwingineko. 

Viongozi hapo wametoa wito kwa viongozi wa kisiasa wa Somali kuendelea na maendeleo yaliyopatikana katika ujenzi wa serikali na siasa shirikishi, hasa uchaguzi na makabidhiano ya madaraka kwa amani, na kutoa rai kwa viongozi wa Somalia kufikisha leo masilahi muhimu ya watu wa Somali kwa amani, huru, haki, na uchaguzi wa kuaminika. 

Wamewasihi viongozi wote wa Somalia, "kujizuia zaidi na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha kuongezeka kwa mvutano." 

Mkutano huo, kwa pamoja umeeleza kuwa AU, EU, IGAD na Umoja wa Mataifa wataendelea kufuatilia kwa karibu hali nchini Somalia.