Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama katika mipaka yetu utaleta maendeleo pembe ya Afrika: Kenya

Balanish Tadese, mmoja  kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya
UNHCR/Rose Ogola
Balanish Tadese, mmoja kati ya Waethiopia 10,000 wanaosaka hifadhi Moyale Kenya

Usalama katika mipaka yetu utaleta maendeleo pembe ya Afrika: Kenya

Amani na Usalama

Amani na usalama ndio msingi wa kila kitu na ni muhimu kila mwanadamu kuchukua hatua ya kuipigania. Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Ugatuzi na sehemu kame wa Kenya, Eugen Wamalwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani.

Akizungumza kandoni mwa mjadala wa wazi  wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliokunja jamvi,  amesema Kenya imebeba mzigo mzito wa wakimbizi kutoka Somalia, Kisa amani na usalama na kuongeza kuwa

“Tayari mataifa yameanza kuzuia wakimbizi. Lakini ukiangali asilimia ya wakimbizi duniani kote, unaona asilimia zaidi ya 80 wako kule Afrika, na Uganda imekuwa na wakimbizi zaidi ya milioni moja, kwa hivyo ni jukumu kubwa sana kuangalia kupigana na mambo ya ugaidi. Lazima tuhakikishe kuna amani Somalia, na amani Sudan Kusini. Kenya iko katikati ya mataifa haya kuyasaidia na ni jukumu ambalo lazima tuendelee kulitekeleza, sababu hata Biblia inasema mpende jirani na ni lazima uhakikishe yuko salama ili na wewe pia uwe salama.”

Na katika mukhtadha huo amesema Kenya imekutana na wa  ujumbe wa Ethiopia  kutafakari mkataba kati ya nchi  hizo mbili kwa lengo la kuzuia ghasia na mbinu za kuleta amani katika Pembe ya Afrika.

“Tumesema lazima tubadili mawazo na será na vilevile tuweke mikakati mipya. Tumesema lazima kwanza tuangalie chanzo cha vita dhidi ya hizi jamii zinakaa mpakani. Wengi wanaokaa mpakani ni wafugaji, na shida ya wafugaji ni nini? Ni maji na malisho. Ukiweza kutatua suala la maji na malisho halafu uboreshe na hali ya wale wenzetu wanakaa mpakani, haijalishi ikiwa huyu ni Mturukana wa Kenya ama wa Uganda, ama wapokoti wa Kenya au wakaramoja wa Uganda. Wote ni wafugaji, wasijali mipaka ili wajali Je ikiwa na kiangazi upande wa Karamoja wanaweza ingia Kenya wapate maji?”