Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gbagbo na Blé Goudé huru, Ntaganda ang’ang’aniwa

Mahakama ya rufaa ya ICC imebaini hakuna mazingira ya kipekee ya kuzuia kuachiliwa huru kwa Laurent Gbagbo na Charles Blé Goudé kutoka kizuizini kufuatia kuchiliwa huru na ICC mwezi Januari mwaka 2019.
ICC
Mahakama ya rufaa ya ICC imebaini hakuna mazingira ya kipekee ya kuzuia kuachiliwa huru kwa Laurent Gbagbo na Charles Blé Goudé kutoka kizuizini kufuatia kuchiliwa huru na ICC mwezi Januari mwaka 2019.

Gbagbo na Blé Goudé huru, Ntaganda ang’ang’aniwa

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mahakama ya rufaa ya mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC leo imetupilia mbali rufaa ya mwendesha mashtaka wa ICC dhidi ya uamuzi wa mahakama hiyo ya kuwaachi huru rais wa zamani wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo na aliyekuwa mkuu wa vijana Charles Blé Goudé.
 

Uamuzi huo wa mahakama ya rufaa ya ICC umepitishwa na majaji watatu huku wawili wakipinga na hivyo Gbagbo na Blé Goudé kuwa huru kwa mujibu wa uamuzi wa ICC wa tarehe 15 mwezi Januari mwaka 2015.
Uamuzi wa sasa ni wa mwisho na Mahakama hiyo ya rufaa imefuta mashart iya kuachiwa huru kwa Gbagbo na Blé Goudé na kuagiza Msajili wa ICC kuandaa taratibu za kuhamishiwa kwa usalama kwa wawili hao kwa nchi ambazo zitawapokea.

Wawili hao, Gbagbo na Blé Goudé walikuwa wanatuhumiwa kuhusika na makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyotendwa nchini Côte d'Ivoire mwaka 2010 na 2011 baada ya uchaguzi.

Majaji watano walikuwa wanasikiliza rufani hiyo ambapo Mwenyekiti wa jopo hilo jaji Chile Eboe-Osuji, amesoma uamuzi mbele ya Gbagbo na Blé Goudé na kutokana na vizuizi vya ugonjwa wa Corona au COVID-19, baadhi ya watu walishiriki wakiwa mahakamani na wengine kwa njia ya mtandao.

Katika uamuzi wake, majaji watatu wamekataa rufani ya mwendesha mashtaka kwa misingi miwili mikuu ya rufani hiyo ya kwamba uamuzi wa Mahakam ya ICC kuwaachilia huru Gbagbo na Blé Goudé mosi; ulikiuka masharti ya sheria na pili ulifanyika bila kuzingatia uthibitisho halali na wa kina wa kuchambua ushahidi.

Mahakama hiyo ya rufaa badala yake imesema kuwa ingawa Mahakama ilipaswa kutoa hukumu na sababu za hukumu hiyo kwa pamoja, kuchelewa kutolewa kwa hukumu na sababu zake haviwezi kuwa sababu ya kufanya mchakato mzima wa kesi kuwa siyo halali. Mahakama hiyo ya rufaa pia imekataa hoja kwamba majaji wawili wa mahakama hiyo ambao ndio waliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya kupitisha uamuzi, walishindwa kuelezea kwa kina na kutumia mara kwa mara suala la uthibitisho pasipo shaka.

Badala yake mahakama ya rufaa imesema kuwa majaji wote wawili walibaini kuwa ushahidi dhidi ya washtakiwa ulikuwa dhaifu.

Majaji waliopinga uamuzi wa mahakama ya rufaa ni Jaji Ibáñez na Jaji Bossa huku Jaji Eboe-Osuji, Jaji Morrison na Jaji Hofmański wakipitisha uamuzi uliowezesha washtakiwa kuwa huru.

John Bosco Ntaganda akiwa mahakamani ICC, The Hague, nchini Uholanzi (picha maktaba)
ICC
John Bosco Ntaganda akiwa mahakamani ICC, The Hague, nchini Uholanzi (picha maktaba)

Ntaganda ang’ang’aniwa, hukumu yake yakaziwa

Katika hatua nyingine, mahakama hiyo ya rufani imekazia hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela dhidi ya kiongozi wa zamani wa waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC John Bosco Ntaganda, hukumu iliyotolewa tarehe 7 Novemba mwaka 2019 na ICC.

Uamuzi wa mahakama hiyo ya rufaa unafuatia hatua ya Ntaganda na mwendesha mashtaka wa ICC kukata rufaa dhidi ya hukumu ya mshtakiwa huyo aliyepatikana na hatia ya makosa 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu jimboni Ituri, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Makosa  18 ambayo ametekeleza ni pamoja na kuhusika na vitendo vya ubakaji na utumwa wa kingono na kuwasajili watoto jeshini, wakiwemo wasichana, makosa ambayo alitenda akiwa kiongozi wa kundi la waasi lililokuwa chini ya Thomas Lubanga, kiongozi wa waasi wa UPC, aliyehukumiwa na ICC mwaka 2012.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo ya rufaa imebaini kuwa Ntaganda hakuonesha kuwa haki yake ya kesi kuendeshwa kwa haki ilivurugwa na pia katika kumhukumu, Mahakama ya ICC haikuzidisha vipengele na mazingira yaliyoelezwa kwenye mashtaka yake.

Mahakama hiyo ya rufaa ya ICC imesema uamuzi wake ni wa mwisho.