Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yawaachia huru Gbagbo na Blé Goudé

Laurent Gbagbo na Charles Blé Goudé wakiwa mahakamani huko The Hague Uholanzi leo tarehe 15 Januari 2019 wakati hukumu ikisomwa. Wameachiwa huru.
ICC-CPI
Laurent Gbagbo na Charles Blé Goudé wakiwa mahakamani huko The Hague Uholanzi leo tarehe 15 Januari 2019 wakati hukumu ikisomwa. Wameachiwa huru.

ICC yawaachia huru Gbagbo na Blé Goudé

Haki za binadamu

Mahakama ya kimataifa ya makossa ya jinai, ICC leo imemwachia huru rais wa zamani wa Côte d'Ivoire Laurent Gbagbo na aliyekuwa mkuu wa vijana Charles Blé Goudé baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasipo shaka mashtaka yote dhidi yao. Arnold Kayanda na taarifa zaidi.

Wawili hao, Gbagbo na Blé Goudé walikuwa wanatuhumiwa kuhusika na makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyotendwa nchini Côte d'Ivoire mwaka 2010 na 2011 baada ya uchaguzi.

Majaji watatu walikuwa wanaendesha kesi hiyo ambapo wawili wao Jaji Cuno Tarfusser ambaye alikuwa kiongozi,  na Jaji Geoffrey Henderson walisema hakuna kesi ya kujibu ilhali jaji Herrera Carbuccia hakuwa na makubaliano yoyote.

Majaji hao wawili wametambua uwepo wa ghasia za kisiasa baada ya uchaguzi wa rais mwaka 2010 huko Abidjan na kwingineko lakini wamesema kuwa mwendesha mashtaka ameshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa Gbagbo na Blé Goudé walitekeleza makossa yaliyokuwa yanawakabili. Hivyo Jaji Tarfusser amesema..

 “Mahakama baada ya kuchambua kwa kina ushahidi wote na kuzingatia hoja zote za kisheria kwa maneno na maandishi kutoka pande zote imebaini kuwa hakuna sababu ya upande wa utetezi kuwasilisha ushahidi zaidi kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha kuhusiana na mashtaka husika. Upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa kulikuwepo mpango wa pamoja wa kumweka madarakani Gbagbo ikiwemo mpango wa mauaji dhidi ya raia.”

Mahakama imeagiza Gbagbo na Blé Goudé waachiliwe huru na kwamba mwendesha mashtaka anaweza kuomba waendelee kusalia rumande kwa sababu maalum.