Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mahakama ya ICC yamtia hatiani Ntaganda kwa uhalifu wa vita

John Bosco Ntaganda akiwa mahakamani ICC, The Hague, nchini Uholanzi (picha maktaba)
ICC
John Bosco Ntaganda akiwa mahakamani ICC, The Hague, nchini Uholanzi (picha maktaba)

Mahakama ya ICC yamtia hatiani Ntaganda kwa uhalifu wa vita

Haki za binadamu

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC leo imemtia hatiani kiongozi wa zamani wa waasi John Bosco Ntaganda kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Bosco Ntaganda, aliyejulikana kwa jina la ''Terminator'', amekutikana na hatia ya makosa 18 ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu ikiwemo makosa ya mauaji, ubakaji na kuwasajili watoto jeshini yaliyotekelezwa Ituri nchini DRC kati ya mwaka 2002-2003.

Majaji Robert Fremr, Jaji Kuniko Ozaki na jaji Chang-Ho Chung walitangaza hukumu hilo mapema leo katika kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa hadharani kwenye mahakama ya ICC iliyoko mjini The Hague Uholanzi.

Majaji hao wamesema Ntaganda,mwenye umri wa miaka  45, ''kiongozi mkuu wa waasi'' alikuwa akitoa amri kuwalenga na kuwaua raia''

Waendesha mashitaka wameongeza kuwa Ntaganda alipanga na kuongoza operesheni ya waasi wa Union of Congolese Patriots (UCP) na tawi lake la kijeshi, la Patriotic Forces for the Liberation of Congo (FPLC).

Amekutwa na hatia ya kuhusika na vitendo vya ubakaji na utumwa wa kingono na pia uhalifu wa kuwasajili watoto jeshini, wakiwemo wasichana. Uhalifu huu ulifanyika wakati Ntaganda alipokuwa kiongozi wa kundi la waasi lililokuwa chini ya Thomas Lubanga, kiongozi wa waasi wa UPC. Aliyehukumiwa na ICC mwaka 2012.

Kwa upande wao mawakili wa Ntaganda wamesem kuwa  Ntaganda mwenyewe ni muathirika kwasababu alisajiliwa jeshini akiwa mtoto.

Ntaganda amekuwa mtu wa nne kuhukumiwa na ICC tangu kuundwa kwake mwaka 2002.

Ntaganda aliyezaliwa mwaka 1973 na kukulia nchini Rwanda alikimbilia nchini DRC baada ya mashambulizi dhidi ya watutsi na kujiunga na jeshi la Congo mwaka 2009  kabla ya kuasi mwaka 2012. Alijisalimisha kwenye ubalozi wa Marekani nchini DRC mwaka 2013.

Kwa mujibu wa majaji wa mahakama hiyo hatua itakayofuata ni kuamua kuhusu kifungo chake na mahakama itapokea mapendekezo kutoka pande zote na washiriki na kisha kutaja tarehe ya kusikiliza hukumu. Hadi wakati huo wa hukumu Ntaganda ataendelea kusalia rumande.

TAGS:ICC, John Bosco Ntaganda, uhalifu wa vita, DRC,