Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yamfunga Bosco Ntaganda, ‘Terminator’ miaka 30 jela

John Bosco Ntaganda wakati hukumu yake ikisomwa mahakamani, leo tarehe 7 Novemba 2019 huko The Hague, Uholanzi.
ICC
John Bosco Ntaganda wakati hukumu yake ikisomwa mahakamani, leo tarehe 7 Novemba 2019 huko The Hague, Uholanzi.

ICC yamfunga Bosco Ntaganda, ‘Terminator’ miaka 30 jela

Amani na Usalama

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC leo imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela kiongozi wa zamani wa waasi John Bosco Ntaganda kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu jimboni Ituri, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Hukumu dhidi ya Bosco Ntaganda, aliyejulikana pia kwa jina la ''Terminator'', imetolewa kwa kauli moja na majaji wote watatu waliokuwa wanaendesha kesi hiyo baada ya kupokea mapendekezo kutoka pande zote na washiriki juu ya kiwango cha hukumu, na pia baada ya kusikiliza mashahidi kuanzia tarehe 17 hadi 20 mwezi Septemba mwaka huu.

Hata hivyo siku ambazo Bosco Ntaganda amekuwa anashikiliwa na ICC kuanzia tarehe 22 Machi 2013 hadi leo tarehe 7 Novemba zitapunguzwa kwenye hukumu  hiyo.

Makosa  18 ambayo ametekeleza ni pamoja na kuhusika na vitendo vya ubakaji na utumwa wa kingono na kuwasajili watoto jeshini, wakiwemo wasichana, makosa ambayo alitenda akiwa kiongozi wa kundi la waasi lililokuwa chini ya Thomas Lubanga, kiongozi wa waasi wa UPC, aliyehukumiwa na ICC mwaka 2012.

Hata hivyo ICC haikupata ushahidi wa pasipo shaka wa madai ya kwamba mshtakiwa  Bosco-Ntaganda alikuwa na ushawishi kwa mashahidi.

Akizungumzia hukumu ya leo, msemaji wa ICC Fadi El Abdallah amesema,

“Upande wa utetezi na mashtaka unaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hii ndani ya siku 30 kuanzia leo iwapo wanaona hakuna uwiano kati ya uhalifu na  hukumu. Halikadhalika kwa mujibu wa Ibara ya 110 kifungu cha 3, cha mkataba wa Roma, mtu anapokuwa ametekeleza theluthi mbili ya hukumu, mahakama itapitia upya hukumu kuona iwapo inapaswa kupunguzwa.”

Kuhusu fidia kwa waathirika na manusura wa vitendo vilivyotekelezwa na mshtakiwa, ICC imesema itashughulikiwa.

Tarehe 8 mwezi Julai mwaka huu, ICC ilimkutana Bosco Ntaganda na hatia pasipo shaka dhidi ya makosa 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu yaliyotekelezwa huko Ituri nchini DRC kati ya 2002-2003.

Majaji waliokuwa wanaendesha kesi hiyo ni Robert Fremr, Kuniko Ozaki na Chang-Ho Chung