Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kifo cha Rais Magufuli: Guterres atuma salamu za rambirambi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa Antonio Guterres (Kulia) akiwa na Rais wa Tanzania John Magufuli kwenye makao makuu ya Muungano wa Afrika Addis Ababa Ethiopia mwaka 2017
UN Photo/Antonio Fiorente
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mastaifa Antonio Guterres (Kulia) akiwa na Rais wa Tanzania John Magufuli kwenye makao makuu ya Muungano wa Afrika Addis Ababa Ethiopia mwaka 2017

Kifo cha Rais Magufuli: Guterres atuma salamu za rambirambi

Masuala ya UM

Kifo cha Rais wa Tanzania John Magufuli kimegusa viongozi mbalimbali ukiwemo Umoja wa Mataifa, mashirika yake na marais na hata viongozi wastaafu.

Salamu za hivi karibuni zaidi za rambirambi zinatoka Umoja wa Mataifa ambako Tanzania ni mmoja wa wanachama.
Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani, ameeleza kushtushwa na taarifa za kifo cha Rais John Magufuli na ametuma salamu za rambirambi kwa familia yake, seriali na wananchi wa Tanzania.

Kupitia mtandao wa Twitter Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO,  Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema, “salamu zangu za dhati za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli. Fikra zangu ziko na familia na taifa wakati huu wa kipindi kigumu.”

Kutoka Somalia, akiandika kwa lugha ya Kiswahili,  Rais Mohammed Farmaajo amesema kwa niaba yake na kwa niaba ya serikali na taifa la Somalia, “ningependa kuwasilisha rambirambi zetu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpoteza kiongozi Rais John Magufuli. Tunalitakia Taifa zima na seriklai Subra na utulivu katika kipindi hiki cha maombi na maombolezo.”

Tweet URL

Nchini Kenya Rais mstaafu Mwai Kibaki kupitia ujumbe wake amesema, “ni  kwa machungu makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Rais wa Tanzania John Magufuli. Natuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki, Tanzania na Afrika Mashariki nzima, naoamba Mungu awapatie faraja katika kipindi hiki.”

Tukisalia Kenya, Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Raila Odinga ambaye alikuwa swahiba wa mwendazake Magufuli, ameelezea kupokea taarifa za kifo kwa huzuni kubwa. “Rais Magufuli na familia yake wamekuwa marafiki wetu wa karibu kwa muda mrefu. Makiwa kwa familia ya hayati na watu wa Tanzania. Mungu ailaze roho yake mahali pema penye wema.”

Na kutoka Uganda, Rais Yoweri Museveni ametuma salamu za rambirambi na kusema, “alikuwa kiongozi wa vitendo aliyeamini na kutekeleza uwezeshaji wa kiuchumi kwa nchi za Afrika MAshariki. Tunaungana na watanzania katika kuomboleza kifo cha mwana huyu wa Afrika aliyetukuka,”

Watanzania nao wapaza sauti- Jua likiniwakia nalisikilizia!

Aurelian Mdulingwa kutoka Dar es salaam amesema “msiba huu nimeupokea kwa majonzi makubwa sana, na hasa nikifikiria jinsi Rais wetu alivyokuwa mtetezi wa wanyonge. Ameweza kusaidia watu waliokuwa wamedhulumiwa, na kuna mambo mengi sana ambayo tulikuwa tunategemea kuwa hii miaka mitano inayokuja atafanya makubwa zaidi. Kwa kweli kwa ujumla mimi nimeona imekuwa pigo kubwa kwangu, kwa watanzania, na hata dunia nzima kwa kuwa walikuwa wanajua ni mtu aliyekuwa anatenda kazi nzuri sana.”

Lilian Valerian Temba anasema amesikitishwa na kifo cha Rais Magufuli akisema, “naona taifa limeporomoka. Ni mtu alitoa uhai wake kwa ajili ya wanyonge. Sijalala usiku wote. Kwa miaka mitano iliyopita amefanya mazuri, miundombinu. Mafanikio yake aliyopanga leo hii Mungu amempenda zaidi.”

Soundcloud

Daniel Yaho mfanyabiashara wa soko la Sinza Afrika Sana jijini Dar es salaam anasema ni pigo kubwa kwa wafanyabiashara kama yeye akisema “hapa nilipo, ni mfano mmoja ambao Rais Magufuli ameniachia mimi kama ukumbusho ambao  ametelekeza yeye katika kipindi cha miaka mitano. Sasa hivi mimi Niko katika soko zuri, jua likiniwakia mimi nalisikilizia nikiwa hapa ndani.”

Tukisalia kwenye osko hilo, Joshua Mgona anasema amepokea taarifa za msiba kwa mshtuko kwa kuwa kile alichosema kwamba ni rais wa wanyonge, walikiona. “Mafanikio alivyosema yeye ni rais wa wanyonge, hata sisi tumeuona, Uongozi wake na utendaji wake wa kazi vinaonekana. Mfano sisi tulikuwa na soko la hovyo, tukaomba msaada tulikuwa tunakaa kwenye mafuriko. Yeye akasema atatujengea soko la kisasa na leo tuko hapa kwenye soko la kisasa tunakaa.”