Hali ya wanawake ni hali ya demokrasia – Kamala Harris
Hali ya wanawake ni hali ya demokrasia – Kamala Harris
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris akihutubia Kikao cha 65 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW65 mjini New York Marekani, amesema "hali ya wanawake ni hadhi ya demokrasia," akiongeza kwamba Marekani imedhamiria kutekeleza maadili ya kidemokrasia yaliyoko katika Azimio la Ulimwengu haki za binadamu.
Aidha Kamala Harris amebaiinisha kuwa anavutiwa na maendeleo yanayofanywa duniani kote katika suala la wanawake na demokrasia na pia anajivunia kwamba,"Hali ya demokrasia pia inategemea kimsingi uwezeshaji wa wanawake. Sio tu kwa sababu kutengwa kwa wanawake katika kufanya maamuzi ni alama ya demokrasia yenye dosari, lakini kwa sababu ushiriki wa wanawake unaimarisha demokrasia. Na hiyo ni kweli kila mahali. Nikiangalia duniani kote, nimeongozwa na maendeleo ambayo yanafanywa. Na ninajivunia kutoa taarifa kwamba, wakati Marekani bado ina kazi ya kufanya, sisi pia, tunapiga hatua na kwamba wanawake wanaimarisha demokrasia yetu kila siku."
Kikao hiki kikiwa kinaelekea kukamilisha wiki yake ya kwanza, kinaupa ulimwengu fursa ya kujadili ushiriki kamili wa wanawake na ufanisi na maamuzi katika maisha ya umma, pamoja na kuondoa ukatili, kwa ajili ya kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote.