Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanawake viongozi yaongezeka lakini usawa wa kijinsia bado changamoto- Ripoti

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa wabunge wa kimataifa katika makao makuu
IPU
Baadhi ya wabunge wa Umoja wa wabunge wa kimataifa katika makao makuu

Idadi ya wanawake viongozi yaongezeka lakini usawa wa kijinsia bado changamoto- Ripoti

Wanawake

Licha ya ongezeko la idadi ya wanawake kwenye ngazi za juu za uongozi wa kisiasa, bado ukosefu wa usawa wa kijinsia umesambaa, limesema toleo jipya la ramani ya wanawake kwenye siasa lililochapishwa na Umoja wa Mataifa na chama cha mabunge duniani, IPU.
 

Ramani hiyo inawasilisha takwimu mpya za nafasi za uongozi kiutendaji, serikali na bungeni ambazo zinashikiliwa na wanawake duniani hadi tarehe 1 Januari mwaka huu wa 2021.

Takwimu zinaonesha nchi zenye idadi kubwa zaidi ya wanawake marais, viongozi wa nchi pamoja na mawaziri.
Hata hivyo, baada ya ongezeko kubwa la mwaka jana la asilimia 21.3 la idadi ya wanawake wanaoshika nafasi za uwaziri, kasi imepungua, ambapo mwaka mwaka huu wa 2021 ongezeko ni asilimia 21.9 tu.

Takwimu pia zinafichua ongezeko la nchi zisizo na wanawake viongozi serikali, na hivyo kurejesha nyumba maendeleo yaliyoshuhudidwa katika miaka michache iliyopita.

Mathalani idadi ya wanawake wabunge mwaka 2021 imeongezeka kidogo sana kwa mujibu wa ripoti ya IPU ya wanawake bungeni iliyozinduliwa wiki iliyopita. Hadi tarehe 1 Januari mwaka huu, idadi ya wanawake kwenye mabunge duniani ilikuwa asilimia 25.5 ikiwa ni ongezeko kidogo kutoka asilimia 24.9 mwaka mmoja uliopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema, “hakuna nchi inayoweza kustawi bila kushirikisha wanawake. Tunahitaji uwakilishi wa wanawake ambao unawakilisha wanawake na wasichana wote kwa utofauti wao, uwezo wao, tamaduni, hali zao za kijamii, kisiasa na kiuchumi. na wasichana wote.”

Wanawake wabunge Afghanistan wakiingia Bungeni (Wolesi Jirga )
UN Photo/Eric Kanalstein
Wanawake wabunge Afghanistan wakiingia Bungeni (Wolesi Jirga )

Bi. Mlambo-Ngcuka amesema ramani ya mwaka huu inaonesha kuwa “bado tunahitaji hatua za kijasiri na za kiuamuzi duniani kote ili kuleta wanawake wengi zaidi katika fursa za kupitisha maamuzi na wao wawe wadau wa kushikiri kikamilifu. Hakuna shaka kuwa hili linaweza na linapaswa kufanyika. Lifanyike sasa.”

Martin Chungong ambaye ni Katibu Mkuu wa IPU akizungumzia ripoti hiyo amesema ongezeko la mwaka huu la idad iya wanawake kwenye nafasi za kupitisha maamuzi ya kisiasa halitoshelezi. “Hasa unapozingatia kuwa asilimia 70 ya wahudumu wa afya na walezi wakati huu wa janga la COVID-19 ni wanawake. Ni juu yetu, wanaume na wanawake kuendeleza kushinikiza uwakilishi mkubwa zaidi wa wanawake kwenye siasa. Tuna mbinu za kuwezesha hilo na tunachohitaji sasa ni utashi wa kisiasa.”

Takwimu hizi mpya zimetolewa kuelekea kuanza kwa mkutano wa 15 wa  hali ya kamisheni ya wanawake duniani, CSW tarehe 15 mwezi huu wa Machi, ikiwa ni kusanyiko kubwa zaidi la wanawake la Umoja wa Mataifa.

Maudhui ya mwaka huu ni “Ushiriki kamilifu na wa kina wa wanawake na utoaji maamuzi kwenye masuala ya umma, na utokomezaji wa ghasia ili kufanikisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana.”

Halikadhalika zimetolewa kuelekea kuanza kwa jukwaa la Kizazi cha Usawa ambalo litawasilisha mabadiliko makubwa katika masuala ya wanawake na uongozi.

Wanawake kwenye uongozi

Kwa mujibu wa takwimu hizi mpya, wanawake wanashika nafasi za urais au uongozi wa serikali katika nchi 22, ikiwa ni ongezeko kutoka nchi 20 mwaka 2020.
Hadi tarehe 1 Januari mwak ahuu aslimia 5.9 ya marais waliochaguliwa ni 9 kati ya 152 ilihali wakuu wa nchi wanawake ni katika nchi 13 kati ya 193.
Ulaya inaongoza kwa kuwa na wanawake wengi zaidi wanaoongoza nchi zikiwemo Denmark, Finland, Iceland, na Norway.

Tweet URL

Kwa kiwango cha mawaziri, idadi imepungua kwa nchi zenye wanawake mawaziri kwa zaidi ya asilimia 50. Idadi imepungua kutoka nchi 14 mwaka 2020 hadi 13 mwaka 2021.

Kwa nchi zenye zaidi ya asilimia 50 wanawake mawaziri ni Nicaragua, 58.82%, Austria 57.14%, Sweden  57.14%, Belgium 57.14%, Albania  56.25%, Rwanda  54.84%, Costa Rica  52.00%, Canada 51.43%, Andorra, Finland, Ufaransa, Guinea-Bissau na Hispani ni 50.00%.

Baadhi ya nchi ingawa hazikufikia asilimia 50 au zaidi, bado zimeongeza idadi ya wanawake mawaziri, mathalani Namibia imeshuhudia ongezeko kubwa kutoka asilimia 15 hadi 39 ya mawaziri wake ni wanawake. Rwanda bado inaongoza katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kwa kuwa na asilimia 54.8 ya mawaziri wanawake huku ikiongoza duniani kwa kuwa na wanawake wengi wabunge.

Kwa Marekani, serikali mpya inaelekea kuwa ni serikali katika historia ya nchi hiyo kwa kuwa na usawa wa jinsia kwenye uongozi. Idadi ya wanawake wanaosimamia wizara imeongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2020 hadi asilimia 46 mwaka 2021.

Hata hivyo idadi ya nchi zisizo na mawaziri wanawake imeongezeka hadi 12 mwaka 2021 kutoka 9 mwaka 2020.

Serikali ambazo hazina kabisa wanawake viongozi ni Azerbaijan, Armenia, Brunei Darussalam, Korea Kaskazini,  Papua New Guinea, Saint Vincent na Grenadines, Saudi Arabia, Thailand, Tuvalu, Vanuatu, Vietnam na Yemen.

Wizara ya Mazingira inaongozwa na wanawake zaidi

Wizara ya mazingira au nishati imeruka kutoka nafasi ya tatu mwaka 2020 hadi kushika nafasi ya juu mwaka 2021 kwa kuwa wizara ambayo inaongozwa zaidi na wanawake.

Mawaziri wanawake wameendelea vilevile kushikilia wizara ya masuala ya jamii, wanawake na usawa wa jinsia.