Kikao cha 65 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW65 chang’oa nanga:UN Women

Mfanyakazi muhamiaji akishona nguo katika moja ya viwanda nchini Thailand kwenye jimbo la Mae Sot
UN Women/Piyavit Thongsa-Ard
Mfanyakazi muhamiaji akishona nguo katika moja ya viwanda nchini Thailand kwenye jimbo la Mae Sot

Kikao cha 65 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW65 chang’oa nanga:UN Women

Wanawake

Kikao cha 65 cha kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW65 leo kimefungua pazia mjini New York Marekani kikishirikisha wadau kutoka kila pembe ya dunia ambao safari hii kwa asilimia kubwa wanashirikia kupitia mtandaoni kwa sababu ya athari na vikwazo vya janga la corona au COVID-19. 

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN-Women kikao hicho kinachofanyika kila mwaka safari hii kitakunja jamvi Machi 26 na mada kuu ni “Ushiriki kikamilifu na wa ufanisi wa wanawake na ufanyaji wa maamuzi katika maisha ya umma, pamoja na utokomezaji wa ukatili kwa ajili ya kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote.” 

Kikao cha mwaka huu pia ni daraja muhimu la kuelekea kwenye “Kongamajo la kizazi chenye usawa” lililoandaliwa na UN women na wenyeji wa kongamano serikali za Ufaransa na Mexico, wakiungana na vijana na asasi za kiraia , na litakuwa fursa muhimu ya kubadili jamii na kuimarisha uongozi wa wanawake wakati huu dunia ikijikwamua kutoka kwenye janga la corona au COVID-19 limesema shirika hilo. 

Kongamano hilo litafungua pazia Mexico City nchini Mexico tarehe 29 hadi tarehe 31 Machi na huko Paris Ufaransa kuanzia tarehe 30 Juni hadi tarehe 2 Julai mwaka huu wa 2021. 

Wanawake vijana waelezea hisia zao kuhusu ukatili wa kijinsia.
© UNICEF/Vinay Panjwani
Wanawake vijana waelezea hisia zao kuhusu ukatili wa kijinsia.

Usawa wa kijinsi bado una demadema 

Kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na UN -Women hivi karibuni mchakato wa kufikia usawa wa kijinsia katika maisha ya umma na katika ufanyaji maamuzi umekuwa ukijikokota sana. 

Kwani hadi sasa duniani kote wabunge wanawake ni asilimia 25% pekee nan chi tatu tu ndio zimefikisha asilimia 50 au zaidi ya wanawake bungeni na wanawake wabunge walio chini ya umri wa miaka 30 ni chini ya asilimia 1%. 

Kwa upande wa wanawake wafanya mazungumzo katika mizozo ni asilimia 13 %, asilimia 6 ya wapatanishi na asilimia 6 ya watia saini katika michakato rasmi ya amani. 

Mwaka 2020 asilimia 7.4 tu ya kampuni tajiri 500 duniani ndio zilikuwa zinaendeshwa na wanawake na ni nchi 22 tu duniani ndizo zinaongozwa na mwanamke. 

Kwa mwenendo huu tunahitaji zaidi ya miaka 100 

UN Women inasema kwa kiwango cha sasa cha maendeleo, itachukua miaka mingine 130 kufikia usawa wa kijinsia katika nafasi za juu za madaraka. 

Na janga la COVID-19 limeathiri wanawake kwa kiasi kikubwa kuanzia kupoteza kazi hadi kuongezeka kwa unyanyasaji dhidi ya wanawake na kazi ya huduma za bila malipo.  

Ingawa wanawake wako mstari wa mbele kupambana na COVID-19 kama wafanyikazi wa huduma ya afya, wavumbuzi na viongozi, michango yao bado haionekani na haithaminiwi sana, limeongeza shirika hilo.  

Asilimia 3.5 tu ya vikosi vya kazi vya COVID-19 katika nchi 87  ndio vimekuwa na usawa wa kijinsia. 

Mwanamke akitembea mji mkonge wa Tripoli, Libya. (maktaba)
UNSMIL/Lason Athanasiadis
Mwanamke akitembea mji mkonge wa Tripoli, Libya. (maktaba)

Mwanamke anaposhika hatamu  

Kwa hivyo, ni nini hufanyika wakati wanawake wanapongoza?  UN Women inasema ushahidi unaonyesha kuwa wakati wanawake wako madarakani, huwekeza katika hatua za sera ambazo mara nyingi hupuuzwa kuanzia kupanua wigo wa huduma za afya na elimu hadi uchumi unaojali mazingira na kutokomeza unyanyasaji dhidi ya wanawake ambayo hatimaye huunda mustakbali endelevu na yenye mnepo. 

Shirika hilo la wanawake la Umoja wa Mataifa limesisitiza kuwa ili kujijenga kutoka kwajanga la COVID-19 kunahitaji wanawake kuwa kitovu katika kuongoza, kufanya maamuzi ambayo yanatumikia sayari dunia, kushughulikia pengo la usawa, na kufikia usawa wa madaraka. 

Kufikia usawa wa kijinsia katika uongozi na kufanya maamuzi inawezekana limesema shirika hilo .  

Upendeleo wa kijinsia katika mabunge na sekta zingine, kutovumilia ukatili, hatua maalum ambazo zinawawezesha wanawake kuingia kwenye nyanja za kisiasa, na kutenga fungu la ufadhili kwa mashirika ya wanawake, kumedhihirika kuwa kichocheo katika kuleta mabadiliko. 

Fuata majadiliano kwenye CSW65, jifunze zaidi juu ya athari za kugawana nguvu sawa, na ni hatua gani zinaweza kutufikisha hapo.