Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yaungana na nchi nyingine zilizopokea chanjo ya COVID-19 kupitia COVAX

Chanjo ya COVAX
© UNICEF Moldova
Chanjo ya COVAX

Somalia yaungana na nchi nyingine zilizopokea chanjo ya COVID-19 kupitia COVAX

Afya

Somalia imejiunga na orodha inayozidi kuongezeka ya nchi zinazopokea chanjo za COVID-19, kupitia mpango wa COVAX baada ya kupokea shehena yake ya kwanza ya chanjo hizo tayari kwa usambazaji nchi nzima.

Shehena ya dozi 300,000 za chanjo ya Oxford-AstraZeneca imewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Abdulle katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kupokelewa mbele ya maafisa wa ngazi ya juu wa Wizara ya Afya wa nchi hiyo pamoja na uongozi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia. 

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan, amewasifu viongozi wa Somalia kwa juhudi zao endelevu za kupambana na coronavirus">COVID-19 na kuahidi kuwa wataendelea kuunga mkono usambazaji wa chanjo nchi nzima ili kudhibiti kusambaa kwa janga la virusi vya corona. Swan anasema,  "Tunahimiza watu kuchukua chanjo. Tunahimiza watu kuendelea na hatua zote zinazoweza kuzuia ugonjwa yaani kunawa mikono, kuvaa mask, na umbali kati ya mtu na mtu. COVID bado ni tishio kubwa. Tunahitaji kukaa macho. Chanjo itasaidia, lakini sio suluhisho pekee.” 

Kundi hili la kwanza la chanjo, kama inavyopendekezwa na Kikosi Kazi cha Kitaifa cha COVID-19, linawalenga wafanyakazi wa mstari wa mbele, wazee na watu walio na magonjwa ya kudumu, hii ikiwa ni jaribio la kupunguza vifo na maambukizi. 

Waziri wa Afya wa Shirikisho la Somalia, Dkt. Fawziya Abikar Nur, amebainisha kuwa chanjo ni njia nzuri ya kukomesha kuenea kwa COVID-19, na kuahidi kuwa dozi zitawafikia walengwa. "Baada ya juhudi bila kuchoka, tumeweza kupokea kundi la kwanza la chanjo na tunatarajia kupokea zaidi. Ningependa kuwashukuru familia yote ya Umoja wa Mataifa kwa kazi kubwa pamoja na Wizara ya Afya ya Shirikisho na Wizara za Afya ya Nchi Wanachama wa Shirikisho." 

Chanjo hizo za kwanza zimefika Somalia ikiwa ni mwaka mmoja kamili tangu nchi hiyo ilipogundua mgonjwa wake wa kwanza wa COVID-19 mnamo Machi 2020. Kufikia sasa, nchi hiyo imerekodi wagonjwa 8,946 waliothibitishwa, pamoja na vifo 349.