Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia yapokea msaada wa chanjo za COVID-19

Mhudumu wa afya akijiandaa kumchoma mhudumu mwingine wa afya chanjo ya COVID-19 kwenye hospitali moja huko Mogadishu nchini Somalia.
© UNICEF/Ismail Taxta
Mhudumu wa afya akijiandaa kumchoma mhudumu mwingine wa afya chanjo ya COVID-19 kwenye hospitali moja huko Mogadishu nchini Somalia.

Somalia yapokea msaada wa chanjo za COVID-19

Afya

Nchi ya Somalia hii leo Agosti 08, 2021 imepokea dozi 108,000 za chanjo ya Corona au COVID-19 kutoka serikali ya Ufaransa kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa ugawaji chanjo za Corona COVAX.

 Akizungumza baada ya kukabidhi chanjo hizo aina ya Oxford/AstraZeneca mjini Mogadishu, balozi wa Ufaransa nchini Somalia Aline Kuster- Menager amesema nchi yake ina nia ya dhati kusaidia wafanyakazi walio mstari wa mbele kupambana na Corona pamoja na watu walio katika hatari zaidi yakupata maambukizi.

“Mpango huu ni sehemu ya kuunga mkono juhudi zinazofanyika ulimwenguni kote kutoka Ufarasa. Rais (wa Ufaransa) Emmanuel Macron ameahidi kutoa dozi milioni 60 za chanjo kabla ya mwisho wa mwaka 2021. Hili ni janga la ulimwengu, na Ufaransa imejitolea kuhakikisha kuna usambazaji sawa wa chanjo ya coronavirus">COVID-19 kote ulimwenguni. Ikiwa tunataka kudhibiti kuenea kwa coronavirus">COVID-19, lazima tushirikiane.”

Waziri wa afya wa Somalia Fawziya Abikar Nur akipokea msaada huo ameshukuru na kusema chanjo zimekuja muda muafaka kwani idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka kwa kasi siku za hivi karibuni. “Njia pekee ya kuzuia kuenea kwa virusi ni kutoa chanjo kwa idadi kubwa ya watu. Tunashukuru kwa msaada huu kutoka kwa serikali ya Ufaransa na natoa wito kwa wote wanaotakiwa kupata chanjo kuhakikisha wanaenda kuchanja.” 

Naye mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Somalia Mohamed Ayoya ameishukuru Ufaransa kwakuhakikisha kuna utoaji sawa wa chanjo.“Msaada huu umekuja wakati unaofaa na utakuwa muhimu katika kuongeza idadi ya watu waliopewa chanjo dhidi ya COVID-19, hasa kwa wafanyakazi wa afya ili waweze kuendelea kutoa huduma muhimu ya afya kwa watoto wa Somalia na familia zao. 

 Takwimu za waliopata chanjo 

Mpaka sasa takriban watu 186,094 wamepata chanjo ya kwanza ya Corona na watu 92,792 wamepata chanjo mbili. 
Somalia inaendelea kutoa kipaumbele katika utoaji wa chanjo kwa wafanyakazi walio kwenye maeneo muhimu kama sekta ya afya, wazee na watu walio na magonjwa sugu ambao wapo hatarini zaidi kuathirika na Corona. 

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO, Dkt. Mamunur Rahman Malik amesema iwapo dunia inataka kumaliza janga hili ni lazima nchi zote kushirikiana.“Ikiwa tunaweza kumaliza janga huku Somalia, tunaweza kumaliza kila mahali. Mfumo dhaifu wa afya nchini, idadi kubwa ya watu, hasa watu walio katika hatari kubwa, bado wanahitaji kupewa chanjo inaweza kufanya virusi kuambukizwa zaidi na tuna hatari ya kutokea kwa aina mpya ya virusi ikiwa hatuwezi kutoa chanjo kwa kasi na viwango.”

 Hali ya Maambukizi 

Tangu mlipuko uanze mwezi Machi mwaka 2020, Somalia imeripoti jumla ya wagonjwa wa Corona 15,735 pamoja na vifo 837 hadi kufikia Julai 24, 2021. 

Mpaka sasa ni asilimia 1.8 ya idadi ya watu nchini Somalia ndio wamepata chanjo kamili, wakati nchi hiyo ikiwa inakabiliwa na changamoto mbili, ya kwanza ikiwa ni kuhakikisha wananchi wake wanapata chanjo, na pili ni kuhakikisha kuna usambazaji sawa wa chanjo hizo kufikia jamii yote.