Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya yaanza kutoa chanjo dhidi ya COVID-19 

Utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Kenya.
WHO Video
Utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 nchini Kenya.

Kenya yaanza kutoa chanjo dhidi ya COVID-19 

Afya

Serikali ya Kenya inaendelea na kampeni ya chanjo dhidi ya corona au COVID-19 baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kupata na kusafirisha dozi zaidi ya milioni moja hadi Nairobi kupitia mkakati wa kimataifa wa upatikanaji wa chanjo COVAX. 
 

Katika hospitali ya taifa ya Kenyatta jijini Nairobi wahudumu wa afya wamekuwa ni miongoni mwa watu wa kwanza kupokea chanjo hiyo aina ya AstraZenica-Oxford  baada ya kufikishwa kwa dozi milioni 1.02 na kuanza kutolewa rasmi mwishoni mwa Juma.  Umoja wa Mataifa uliwakilishwa na mratibu mkazi wake nchini Kenya Stephen Jackson.

Bwana Jackson amesema, “niko hapa kwenye hospitali ya taifa ya Kenyatta ambako nimeshuhudia tukio la kihistoria , serikali ya Kenya ikizindua kampeni ya kitaifa ya chanjo dhidi ya COVID-19 na nimeshuhudia kwa macho yangu wahudumu wa afya wakipatiwa chanjo hiyo, nimeona wagonjwa pia, umekuwa ni waakati wa kihistoria unaogusa hata kukufanya ulengwe na machozi, tumeanza kuona mwanga katika giza totoro na Umoja wa Mataifa unashiriki kwa kila hali.” 

Mratibu huyo amewachagiza wahudumu wa afya wajitokeze kwa wingi kupokea chanjo hiyo muhimu kwani taifa linawategemea kuifikisha mahali waliko wananchi. 

Shehena ya chanjo hiyo yan AstraZenica iliwasili Nairobi tarehe pili Machi kwa msaada wa UNICEF kupitia shirika la ndege la Qatar na kisha kupelekwa hadi katika bohari kuu ya chanjo na hatimaye hospitali kuu ya taifa ya Kenyatta tayari kwa uzinduzi wa kampeni ya chanjo iliyoanza mwishoni mwa wiki. 

Waziri wa afya wa Kenya Mutahi Kagwe ameishukuru UNICEF, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na muungano wa chanjo duniani GAVI kwa kufanikisha hatua hiyo ya kihistoria ya kuwasili kwa shehena ya kwanza ya chanjo ambayo amesema itaokoa maisha ya watu wengi. 

Wizara ya afya ya Kenya imesema imeweka mpango maalum wa ugawaji wa chanjo hiyo ikianza na wahudumu wa afya na wafanyakazi wengine wa muhimu kama wa ulinzi na usalama. 

Chanjo hiyo ambayo kwa sasa inahifadhiwa katika bohari kuu ya taifa ya chanjo itagawanywa katika vituo tisa vya kikanda vya chanjo ambako hospitali zitachukua na kusambaza katika kaunti mbalimbali na kila kaunti itakuwa na kituo maalum cha chanjo. 

Kenya imepangiwa kupokea dozi milioni 3.56 kupitia mkakati wa COVAX na zaidi ya hapo UNICEF imetoa kwa nchi hiyo mabomba ya sindano milioni 1,025,000 na maboksi salama 10, 250 ya kuhifadhia mabomba hayo. 

Naye mwakilishi wa UNICEF nchini Kenya Maniza Zaman amesema kuanza kwa kampeni hiyo ya chanjo Kenya inamaanisha UNICEF na wadau wake wanatimiza ahadi ya COVAX ya kuhakikisha watu kutoka katika nchi zisizojiweza hawaachwi nyuma katika mchakato wa kimataifa wa chanjo hiyo ya kuokoa maisha.