Ninajiandaa kwa ajili ya nafasi kubwa katika maisha haya.

27 Februari 2019

Kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za utamaduni, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa bado kuna umuhimu wa kuweka mazingira ya kuwahamasisha wasichana kujiunga katika fani za sayansi. Fatima Khamis kutoka Sudan ni mwanamke pekee katika kitengo cha uhandisi wa mitambo ya mawasiliano ya walinda amani walioko chini Jamhuri ya Afrika ya kati.

Katika nchi hiyo ambayo imeghubikwa na ukosefu wa usalama kwa muda mrefu, kuna zaidi ya walinda amani 13,000 wanaosaidia kurejesha amani na utulivu lakini ni asilimia 5 pekee ambao ni wanawake.

Mmoja wa wanawake hao wachache ni Fatima Khamis ambaye baada ya panda shuka katika minara mirefu ya mawasiliano sasa yuko ofisini kwake akipokea na kutoa maelekezo kwa njia ya simu.

Fatima alijiunga na mpango wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa huko Afrika ya kati MINUSCA akifanya kazi kama mhandisi wa mtandao wa intaneti. Anasema alikokulia ni kama vile elimu ilikuwa maalumu kwa wavulana tu.

“Kazi hizi zote zimesheheni wanaume na kunapokuwa na mwanamke, wanafikiri hawezi, ili kuibadili dhana hii tunatakiwa kufanya kazi sana.”

Fatima anasema mwanzo alipojiunga na shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP walikuwa wanawake sita tu katika chumba cha redio na alipohamia katika kikosi cha sasa, yeye ni mwanamke peke yake. Hivi sasa Fatima anataka kutengeneza jina lake katika fani hii ya uhandisi wa mitandao ya mawasiliano.

“Kama unavyofahamu, hii fani inabadilika haraka sana. Ninatakiwa kusoma sana. Nimeanza masomo yangu ya uzamili baada ya kujiunga na kazi hii na sasa nusu ya masomo yangu imeshakamilika. Ninajiandaa kwa ajili ya nafasi kubwa katika maisha haya.”

 Kama ilivyo kwa Fatima, wengi wa wanawake wanaofanya kazi katika Umoja wa Mataifa wanafungua mianya mipya katika teknolojia ya habari.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud