COVID-19 imeongeza pengo la usawa wa kijinsia kwa wakimbizi wanawake na wasichana:UNHCR

8 Machi 2021

Athari za janga la COVID-19 zinatishia maisha na haki za wakimbizi, wanawake na wasichana wasio na makazi, limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi NHCR, wakati ikiadjimishwa Siku ya wanawake duniani. 

Kamisha mkuu wa UNHCR Filipo Grandi amesema “Athari hizo ambazo ni za kiuchumi na kijamii hazijawahi kutokea na zinayaacha Maisha ya watu wengi katika hatari kubwa.Tunashuhudia kuongezeka kwa ripoti za unyanyasahji wa kijinsia, pamoja na unyanyasaji wa majumbani, ndoa za kulazimishwa, utumikishwaji wa watoto na mimba za utotoni.” 

 Hizi zinahusishwa na kuongezeka kwa shinikizo za kijamii na kiuchumi, kuongezeka kwa mivutano katika majumbani na katika jamii na kufungwa kwa shule, zote zikisababishwa na umaskini unaohusiana na janga la COVI-19. Ameongeza Bwana Grandi. 

 Pia amesema baadhi ya manusura hata wanaamua kuchukua hatua kali ya kuondoa malalamiko yao kwa sababu ya utegemezi wa kiuchumi kwa wenzi wanyanyasaji. 

Polisi wa UNAMID wakiwezesha mafunzo ya lugha ya kiingereza kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini El Fasher , Kaskazini mwa Darfur Sudan
UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Polisi wa UNAMID wakiwezesha mafunzo ya lugha ya kiingereza kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini El Fasher , Kaskazini mwa Darfur Sudan

Pengo la usawa linapanuka 

"Tunashuhudia dhihirisho kubwa la ukosefu wa usawa wa kijinsia kwa baadhi ya watu walio katika mazingira hatarishi zaidi na walio katika mazingira magumu na mmomonyoko wa kutisha wa hatua muhimu zilizokwishapigwa katika usawa wa kijinsia miongo michache iliyopita," amesema Grandi. 

Ameongeza kuwa “Jumuiya ya kimataifa lazima ichukue hatua na kusaidia kulinda haki za wanawake na wasichana waliolazimika kutawanywa na wasio na utaifa. Hii inahitaji msaada kwa mipango ya kibinadamu inayopambana na pengo la usawa wa kijinsia, ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, na pia kuongeza wigo wa elimu,  mipango ya ufundi na kujitegemea. Ni muhimu kwamba wanawake na wasichana hao pia wajumuishwe katika mipango ya misaada ya kijamii na kiuchumi inayowekwa na kutekelezwa na serikali. ” 

 
IOM ikitoa msaada kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini Baghdad Iraq
Picha: IOM
IOM ikitoa msaada kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini Baghdad Iraq
Asilimia 85 ya wakimbizi wote duniani wanahifadhiwa katika mataifa yanayoendelea na kwa kiasi kikubwa wanategemea misaada ya kibinadamu au vibarua vya kutwa.  

Wengi sasa wamepoteza uwezo wa kujimudu kimaisha na wametumbukizwa katika umasikini wa kutisha na athari mbaya na kubwa. 

 "Pamoja na kuongezeka kwa hatari za machafuko, unyanyasaji, unyanyasaji wa kijinsia na usafirishaji haramu wa binadamu, vyote vikiwa ni matokeo ya kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia, athari za janga la COVID-19 pia zinathibitisha maafa katika elimu ya wasichana wa wakimbizi. Wasichana wengi wanalazimika kuacha shule na kufanya kazi, kuuzwa au kuolewa, " kwa mujibu wa mkuu wa ulinzi wa UNHCR, Gillian Triggs. 

Wasicha milioni 13 hatarini kwa ndoa za utotoni 

UNHCR inasema wakati washirika wa masuala ya kibinadamu wanakadiria kuwa wasichana zaidi ya milioni 13 sasa wako katika hatari ya kuolewa kwa kulazimishwa kutokana na janga COVID-19, ndoa za utotoni tayari zinageukiwa na familia zingine za wakimbizi ambazo zimeghubikwa na kudhoofishwa na umasikini. 

Shirika hilo limeongeza kuwa wanawake wakimbizi pia wanaelemewa na mzigom wa kutoa huduma na utunzaji wa ziada majumbani, wakigeukia kazi za hatari katika sekta isiyo rasmi, au mitaani.  

Wanawake wakimbizi wa ndani UAE wakijipanga kupokea msaada wa chakula kutoka Shirika la Msalaba mwekundu la UAE (Picha ya Maktaba)
UN/ Tobin Jones
Wanawake wakimbizi wa ndani UAE wakijipanga kupokea msaada wa chakula kutoka Shirika la Msalaba mwekundu la UAE (Picha ya Maktaba)

Pia janga hilo la corona limeongeza mahitaji ya kaya na kunapunguza fursa zao za elimu nah uku wakiwa katika hatari kubwa ya maambukizi ya virusi hivyo. 

Triggs amesisitiza kwamba "Ulemavu, kutengwa, mwelekeo wao wa  kijinsia na utambulisho wao wa kijinsia pia vinazidisha ubaguzi na hatari za unyanyasaji kwa wanawake na wasichana wakimbizi, wasio na makazi, waliotawanywa na wasio na utaifa."  

 Ameongeza kuwa licha ya janga la COVID-19 kuchochea kukosekana kwa usawa wa kijinsia na kuongeza hatari za unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana, mipango ya kuzuia na kukabiliana nao bado haijapata ufadhili wa kutosha.
UNHCR inasisitiza tahadhari kuchukuliwa mara moja na serikali kwa hatari hizi na kuunga mkono ushiriki kamili na uongozi wa wanawake wakimbizi, waliotawanywa na wasio na utaifa katika mipango ya kukabiliana na kujikwamua na janga hilo.
 

Kushiriki kikamilifu na kwa maana kwa wanawake na wasichana katika maamuzi ambayo yanaathiri maisha yao, familia na jamii zao ni muhimu katika kudumisha haki zao za binadamu, kuhakikisha ulinzi wao imara na kusaidia uwezeshwaji wao. 

"Hadi pale juhudi za pamoja zitakapofanyika kupunguza athari za kijinsia za COVID-19, tuna hatari ya kuwaacha nyuma wanawake na wasichana wakimbizi, waliotawanywa na wasio na uraia," amesema Triggs.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter