Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani wanawake TANZBATT_13 watia nuru Darfur 

Walinda amani wa Tanzania wanaohudumu chini ya UNAMID, Darfur, Sudan.
UNAMID
Walinda amani wa Tanzania wanaohudumu chini ya UNAMID, Darfur, Sudan.

Walinda amani wanawake TANZBATT_13 watia nuru Darfur 

Amani na Usalama

Kuelekea siku ya wanawake duniani tarehe 8 mwezi huu wa Machi, leo tunakwenda huko Menawash, jimboni Darfur nchini Sudan ambako kumuangazia mlinda amani mwanamke kutoka Tanzania anayehudumu kwenye kikosi cha 13 cha Tanzania, TANZBATT_13 katika ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika UNAMID anaelezea kile alichofanya kuinua wanawake na wasichana nchini humo.  

Afisa mteule daraja la pili Modesta Gwido Mpulule ameeleza ushiriki wake katika majukumu ya ulinzi wa amani na mahusiano kati ya walinda amani wanawake na wanawake wakimbizi wa ndani.  

Modesta ambaye amekuwepo kwa miezi 21 huko Menawash amesema "tulipofika mahali hapa tulikuta wakazi wa eneo hili la Menawash, suala la kumpeleka mtoto shule kwao sio kitu cha muhimu. Katika maeneo yetu ya uwajibikaji, wazazi wamekuwa wakiruhusu watoto wao wasiende shule na badala yake waolewe.” 

Amesema kwao hawakukata tamaa bali waliamua kutoka elimu kwa kuwa suala hilo linatokana na mila na desturi za Menawash,  “hivyo tulianza kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo haya walioathirika na vita vya wenyewe kwa wenyewe lengo wajue umuhimu wa kumpeleka mtoto shule badala ya kumpeleka mtoto kwenda kuchunga ngamia, kufanya shughuli za shamba pamoja na nyumbani. Halikadhalika tulitoa elimu mara kwa mara kuhusu madhara za ndoa za utotoni.” 

Kilichokuwa kinamtia moyo mlinda amani huyu wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania ni kwamba, “kama mzazi kinachonitia moyo kwa muda wa miezi 21 niliyohudumu hapa, kuanzia siku ya kwanza tumeanza kutoa elimu kwa wazazi na walezi wameanza kutuelewa na kuipokea elimu yetu na sasa watoto wameanza kwenda shule na wanafanya vizuri katika masomo yao.” 

Mwakilishi wa umoja wa vikundi vya wanawake katika kijiji cha Menawash,  Sandra Mohamed Ali ametoa shukrani kwa wanawake walinda amani wa kikosi cha TANZBATT 13 kipindi chote walichohudumu majukumu ya ulinzi wa amani katika eneo hilo.  

Bi. Sandra amesema, “nawashukuru wanawake wa TANZBATT 13, tumeshirikiana pamoja, wamekuwa wakitupa elimu mbalimbali katika jamii yetu na wameendesha madarasa ili tuendelee kuwa salama. Tangu kuwepo watanzania eneo hili hakujatokea vita na hakuna kitu chochote cha kuhatarisha amani katika mji wetu ndio maana hadi leo tunaishi salama. Kwa sasa UNAMID inaondoka, tunawashukuru sana wanawake wa TANZBATT 13 na sasa tutashirikiana sisi wenyewe ili kuujenga mji wetu.”