Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANZBATT_13 wapatiwa mafunzo dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia 

Wanawake  Darfur
Nawal Hassan
Wanawake Darfur

TANZBATT_13 wapatiwa mafunzo dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia 

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umeweka bayana kuwa katu hauvumilii vitendo vyovyote vile vya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa kingono iwe vimetekelezwa na mfanyakazi wake au mlinda amani anayewakilisha taifa lake chini ya bendera ya chombo hicho chenye wanachama 193. 

Ni kwa mantiki hiyo katika mipango ya ulinzi wa amani mafunzo hufanyika ili kuzingatia maadili kama ilivyofanyika kwa walinda amani wa kikundi cha 13 cha Tanzania kwenye ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, UNAMID jimboni Darfur nchini Sudan. 

Darasa la hivi karibuni zaidi limefanyika Khor Abeche jimboni Darfur nchini Sudan na wanafunzi walikuwa ni walinda amani wa TANZBATT 13. 

Wameongezewa ufahamu kuhusu madhara ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia na  ukatili wa kingono kwa wanawake na watoto ili kuepuka vitendo hivyo wanapokuwa kwenye majukumu ya ulinzi wa amani . 

Mafunzo haya hutolewa kila baada ya siku 90 na washiriki takribani 84 wamenufaika na yamefanyika kwa siku mbili. 

Afisa uhusiano na Polisi jamii UNAMID kambini Khor Abeche Daisle Simon Ulomi ndiye alikuwa mkufunzi ambapo amesema, “mafunzo ya unyanyasaji wa kijinsia, na ukatili wa kingono wanayotoa husaidia kuongoza mienendo ya walinda amani wanapokuwa kwenye majukumu yao. Mafunzo haya ni sehemu muhimu na husaidia walinda amani kuendelea kujiweka salama na kutojihusisha na vitendo vya kingono, udhalilishaji na unyanyasaji.” 

Sajenti Athumani Mleche ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo na amesema amefarijika na mafunzo waliyopatiwa, “Natoa wito kwa UNAMID na wafanyakazi wake kuendelea kutoa mafunzo haya kwa sababu  yanatufanya tuwe na uelewa zaidi katika utendaji wa kazi za kila siku.” 

Vikosi vya Tanzania vimekuwa vinahudumu UNAMID kwa takribain miaka 10 sasa ambapo TANZBATT_13 iliyoanza jukumu lake mwezi Mei mwaka 2019 inatarajia kutamatisha shughuli zake mwakani.