Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANZBATT-13 yakabidhi jengo la madrasa Khor Abeche 

Walinda amani kutoka Tanzania kwenye UNAMID huko Darfur.
UNAMID/TANZBATT_13// Koplo Japhet Chaula
Walinda amani kutoka Tanzania kwenye UNAMID huko Darfur.

TANZBATT-13 yakabidhi jengo la madrasa Khor Abeche 

Amani na Usalama

Huko jimboni Darfur nchini Sudan , walinda amani kutoka Tanzania kwenye ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika wa kuweka utulivu jimboni Darfur, (UNAMID) wamekabidhi kwa wakazi wa Khor Abeche jengo jipya la madrasa. 

Walinda amani hao wa kikosi cha TANZBATT-13 walianza harakati za ujenzi wa madrasa hiyo kwa kushirikiana na wakazi wa eneo hilo ambapo pia waliwafundisha jinsi ya kufyatua matofali. 

Vifaa vya ujenzi yakiwemo mabati yalinunuliwa na walinda amani hao sambamba na ujenzi kufanywa na walinda amani lengo likiwa ni kujenga uhusiano mwema na wakazi hao sambamba na kuwezesha watoto wa wakazi wa Khor Abeche kupata elimu ya dini yao katika mazingira bora. 

Kiongozi wa dini ya kiislamu katika eneo Mohamed Abubakar akizungumza wakati wa makabidhiano ya madrasa hiyo amesema, « leo sisi ni mashahidi, siku yenye heri kwa sababu leo tumefungua madrasa ya kufundisha Quran kwa ajili ya watoto  wetu wanaoishi Khor Abeche. Hili ni jambo bora walilofanya askari wa TANZBATT- 13 katika eneo letu la khor abeche. » 

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Khor Abeche na TANZBATT_13

Ameongeza shukrani zake akisema kwao ni jambo kubwa na la furaha « kwa binadamu kufanya kitu kitakacholeta faida duniani na ahera. Sisi nasi tunaweka ahadi ya kusimamia na kulihifadhi hili jengo la madrasa kwa ajili ya kufundisha watoto wetu misingi ya sheria ya dini ya kiislamu ambayo watoto wetu wanatakiwa kujua kwa ajili yamaisha yao ya baadaye.” 

Bwana Abubakar amemshukuru pia kamanda wa kikosi Tanzbatt - 13,  Luteni Kanali Khalfani Rashid Kayage na uongozi wa kikosi, na kila aliyeshiriki kujenga jengo hilio. 

TANZBATT 13

Kikosi hicho cha 13 cha Tanzania huko UNAMID nchini Sudan kimekuwepo huko tangu tarehe 16 mwezi Mei mwaka 2019 na kinatarajia kukamilisha jukumu lake mwezi Machi mwakani.

TANZBATT 13 ina jumla ya wanajeshi na askari 324 ambapo kinahusika na ulinzi wa raia na kambi zake ziko Khor Abeche, Minawashi na El Fasher.

UNAMID imekuwepo Darfur Sudan tangu mwaka 2007 kufuatia azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Julai mwaka 2007. 

UNITAMS

Awali operesheni zake zilikuwa zifungwe mwaka huu lakini zikaongezewa muda wa miezi miwili kuanzia Oktoba  hadi Desemba 31 mwaka huu wa 2020 na itakabidhi shughuli zake kwa ujumbe wa usaidizi kwa Sudan UNITAMS. 

UNITAMS imeanzishwa kwa azimio namba 2524 la tarehe 4 Juni mwaka huu wa 2020 na kirefu chake ni United Nations Integrated Transition Assistance Mission in Sudan. 

Jukumu lake kuu ni kutoa usaidizi wa kiufundi katika mchakato wa kutunga katiba, kusaidia utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, usawa, uwajibika na usimamizi wa vipengele vya utawala wa sheria kwenye nyaraka ya katiba.