Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wa shule 300 watekwa nyara Nigeria, UNICEF yalaani

Mtoto wa kike akiwa darasani kwenye moja ya shule za msingi nchini Nigeria
© UNICEF/Apochi Owoicho
Mtoto wa kike akiwa darasani kwenye moja ya shule za msingi nchini Nigeria

Watoto wa shule 300 watekwa nyara Nigeria, UNICEF yalaani

Amani na Usalama

Hii leo katika jimbo la Zamfara kaskazini-magharibi mwa Nigeria, zaidi ya watoto 300 hawajulikani waliko baada ya watu wenye silaha kushambulio shule yao, tukio ambalo limelaaniwa vikali na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Nigeria Peter Hawkins amenukuliwa katika taarifa ya shirika hilo akisihi wateka nyara hao kuwaachia mara moja watoto hao.

“Tunachukizwa na kusikitishwa na tukio lingine tena la kutekwa watoto wa shule nchini Nigeria. Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto na ni uzoefu wa kutisha ambao wanapitia, uzoefu ambao unaweza kuwa na madhara makubwa na ya muda mrefu kwa afya ya akili na ustawi wao,” amesema Bwana Hawkins.

Maisha ya kawaida

“Matukio kama hayo yamekuwa vitu vya kawaida kwa watu wengi wa Nigeria” alinukuliwa Bwana Hawkins katika mahojiano na  UN News, kabla ya tukio la leo.

Wahalifu ambao wana lengo la kujipatia fedha haraka kwa kulazimisha familia au mamlaka kuwalipa fedha ili waweze kuwaachilia huru mateka wao na mara nyingi wanalenga taasisi ambazo ziko mbali kufikiwa na mamlaka, alieleza Bwana Hawkins.

Tukio la leo limefanyika wakati makumi ya wavulana na walimu wakiwa wametekwa kutoka jimbo la kati la Niger nchini Nigeria wiki iliyopita, na hadi leo hawajaachiliwa huru.

Baada ya miaka miwili ya kushikiliwa na kundi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria, mmoja wa wasichana wa Chibok akieleza hali mbaya aliyokutana nayo.
UNICEF Nigeria
Baada ya miaka miwili ya kushikiliwa na kundi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa Nigeria, mmoja wa wasichana wa Chibok akieleza hali mbaya aliyokutana nayo.

Shambulio la usiku

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, shambulio la leo Ijumaa limefanyika usiku wa manane katika shule ya sekondari ya wasichana ya Jangebe jimboni Zamfara.
“Tunalaani vikali shambulio hili na tunatoa wito kwa watekelezaji kuwaachia huru watoto hao wa kike mara moja na kwa serikali kuchukua hatua kuhakikisha wanaachiliwa huru wakiwa salama na usalama wa watoto wote wa shule nchini Nigeria,” amesema Bwana Hawkins katika taarifa ya leo.

Amesema watoto wanapaswa kujisikia salama wakati wote iwe nyumbani au shuleni na kwamba wazazi hawapaswi kuwa na hofu asubuhi pindi watoto wao wanapoondoka nyumbani kuelekea shuleni.

Baada ya kutambua juhudi za serikali ya Nigeria ya kuhakikisha watoto hao wanaachiwa huru salama, UNICEF imesihi pia mamlaka hizo kuhakikisha maeneo ya shule yanakuwa salama.

Kitisho cha Boko Haram

Pamoja na magenge ya uhalifu yanayoendesha operesheni zao kaskazini-magharibi mwa Nigeria, Kaskazini-Kati na kaskazini-mashariki, magaidi wa Boko Haram bado wanadhibiti maeneo makubwa ya eneo la Kaskazini-Mashariki.

Takribani miaka saba iliyopita, Boko Haram ambao jina hilo linamaanisha, Elimu ya Kimagharibi ni marufuku, waliteka nyara wanafuzi wa kike 276 wa eneo la Chibok kaskazini-magharibi mwa Nigeria na hadi leo wengi wao hawajulikani waliko.

Elimu ni ufunguo

Licha ya hatari, watetezi wa haki za binadamu wanaamini kuwa elimu inapaswa kusalia kipaumbele cha serikali na inapaswa kuhakikisha hata walio hatarini wanaipata haki hiyo.

Akiangazia hatua zilizochukuliwa dhidi ya ngome ya Boko Haram, huko Maiduguri, mji mkuu wa jimbo la Borno, Bwana Hawkins ameelezea furaha aliyonayo kuona maelfu ya watoto sasa wamerejea shuleni kitu ambacho kilikuwa ndoto mwaka 2009 mashambulizi ya kundi hilo yalipoanza.

Mabadiliko ya kimiujiza yanawezekana

“Iwapo ungalienda Maiduguru mwaka 2015-2016 hakuna kitu kilichokuwa kinafanyika, hakuna shule,” amesema Hawkins lakini hivi sasa kuna msururu wa vyombo vya usafiri vikisafirisha wanafunzi wasichana na wavulana akisema hayo ni mabadiliko ya kimiujiza.