Umoja wa Mataifa walaani vikali shambulio na utekaji wanafunzi Nigeria. 

18 Februari 2021

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kupitia msemaji wake, amelaani vikali shambulio la tarehe 17 Februari mwaka huu 2021 dhidi ya Chuo cha Sayansi cha serikali cha Kagara katika mkoa wa kaskazini kati mwa Nigeria. 

Kwa mujibu wa Msemaji wa Guterres, taarifa kutoka Nigeria zimeeleza kuwa  tukio hilo limesababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na kutekwa nyara kwa watoto wengine wa shule, jamaa na wafanyakazi. Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na kwa familia zilizoathiriwa. 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba mashambulizi dhidi ya shule na vituo vingine vya elimu ni ya kuchukiza na hayakubaliki. 

"Katibu Mkuu anatoa wito kwa mamlaka ya Nigeria kutoacha kila juhudi katika kuokoa waliotekwa na kuwawajibisha wale waliohusika na kitendo hicho.” Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric ameewaeleza wanahabari.  

UNICEF Nigeria 

Naye Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Nigeria, Peter Hawkins akizungumza kuhusu shambulio hilo amesema, “UNICEF inafahamu kwamba usiku, watu wenye silaha wameshambulia Chuo cha Sayansi cha serikali huko Kagara, katika Jimbo la Niger, Nigeria. Kwa mujibu wa ripoti ambazo hazijathibitishwa, wanafunzi wengi hawajulikani waliko, ingawa bado haijafahamika ni wangapi.” 

Kiongozi huyo pia amelaani vikali shambulio hilo dhidi ya shule na kutoa wito wa kuwaachia haraka pasina masharti, watoto wote ambao hawafahamiki waliko, na warejeshwe nyumbani kwao wakiwa salama katika familia zao. 

Bwana Hawkins ameongeza kusema, “UNICEF ina wasiwasi mkubwa kuhusu vitendo hivi vya ghasia vilivyoripotiwa. Mashambulio kwenye shule ni ukiukaji wa haki za watoto. Watoto wanapaswa kujisikia wako salama nyumbani na shuleni wakati wote na wazazi hawapaswi kuhofia usalama wa watoto wao wakati wanapowapeleka shuleni asubuhi.” 

Hata hivyo kiongozi huyo wa UNICEF nchini Nigeria ameipongeza Serikali ya Nigeria kwa juhudi inazozichukua kuwarejesha kwa usalama watoto wasiojulikana waliko.  

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter