Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnyumbuliko mpya wa virusi vya COVID-19 watia hofu juu ya ufanisi wa chanjo- WHO

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19
UN Photo/Evan Schneider
Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumza katika moja ya taarifa za WHO kuhusu janga la COVID-19

Mnyumbuliko mpya wa virusi vya COVID-19 watia hofu juu ya ufanisi wa chanjo- WHO

Afya

Kuibuka kwa mnyumbulio wa virusi vya Corona au COVID-19 umeibua wasiwasi na maswali iwapo chanjo zilizopo hivi saa zina uwezo na ufanisi dhidi yao, amesema Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya Afrika Kusini kutangaza kusitisha kwa muda utoaji wa chanjo dhidi ya Corona au COVID-19 aina ya Oxford-AstraZeneca.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Dkt. Tedros amesema “uamuzi wa serikali ya Afrika Kusini umefanyika baada ya uchunguzi kubaini kuwa chanjo hiyo Oxford-AstraZeneca haina ufanisi katika kuzuia ugonjwa wa Corona usababishwao na aina mpya ya mnyumbuliko mpya wa COVID-19 iliyopatikana Afrika Kusini.”

Hata hivyo amesema kuna maonyo ambayo yalitolewa kuhusu chanjo hiyo kwa kuzingatia ‘kiwango kidogo cha watu waliotumika kwenye majaribio ya chanjo na umri mdogo na afya ya walioshiriki majaribio ya chanjo hiyo. Ni muhimu kutambua iwapo chanjo hiyo bado ina uwezo au haina uwezo wa kuzuia zaidi ugonjwa.”

Profesa Salim Abdool Karim, Mwenyekiti mwenza wa kamati ya ushauri ya mawaziri kuhusu COVID-19 amesema “uchunguzi uliangalia maambukizi ya kiwango kidogo na cha kati na si kwa sababu hawakuwa wanatarajia kufifishwa kwa virusi lakini ni kwasababu ya kiwango ambacho virusi hivyo vilififishwa. Kwa hiyo sasa hatufahamu na hatuna uhakika kuhusu ufanisi wa chanjo hiyo katika kuzuia wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na COVID-19. Tunafahamu kutoka katika majaribio ya ujumla kuwa AstraZeneca inauwezo wa kukabili minyumbuliko mingine ya virusi vya Corona, lakini hatuna imani na chanjo hiyo kwenye mnyumbuliko aina ya 501Y.V2."

WHO kutangaza uamuzi wake

Dkt. Tedros amesema wataalamu wa WHO wanatarajia kufanya uamuzi katika siku chache zijazo kuhusu kuorodheshwa kwa chanjo hiyo kwenye orodha ya chanjo za dharura kwa kuwa India na Korea Kusini zilikuwa zitengeneze chanjo hizo kwa ajili ya jukwaa COVAX linaloratibu usambazaji wa chanjo hizo.

“Tumejizatiti kutumia tathmini zote zilizopo. Lakini kwa sasa COVAX itaendelea kuandaa usambazaji wa robo ya kwanza ya mgao wake na pia kuendelea kuimarisha hifadhi yake ya chanjo,” amesema Dkt. Tedros.