Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maneno matupu hayavunji mfupa, ni wakati wa vitendo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:UN 

Viwango vya hewa ukaa vinaendelea katika kiwango cha rekodi ya juu, licha ya kushuka kwa uchumi kusababishwa na janga la COVID-19.
Unsplash/Johannes Plenio
Viwango vya hewa ukaa vinaendelea katika kiwango cha rekodi ya juu, licha ya kushuka kwa uchumi kusababishwa na janga la COVID-19.

Maneno matupu hayavunji mfupa, ni wakati wa vitendo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi:UN 

Tabianchi na mazingira

Nchi zinazowakilisha asilimia 70 ya uchumi wa dunia na wachangiaji wa asilimia 65 ya hewa ukaa sasa zimeahidi ushiriki wao katika kutokomeza kabisa hewa ukaa. 

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo katika ujumbe wake kwa mkutano ulioandaliwa na Rais wa mkutano wa 26 wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 kwa nchi wanachama. 

Ni miezi tisa iliosalia kabla ya mkutano huo wa kihistoria utakaofanyika mjini Glasgow nchini Uingereza kwa lengo la kusongesha juhudi za kuepuka zahma ya mabadiliko ya tabianchi. 

Hatua zinazochukuliwa hazitoshi 

Guterres amesema muungano wa wamiliki wa samani zisizozalisha hewa ukaa ambao unawakilisha zaidi ya dola trilioni 5 umeahidi kuongeza mara mbili ukubwa wa kundi hilo ifikapo wakati wa mkutano wa COP26, na kuongeza kuwa huu ni mchakato muhimu lakini hautoshi kwani “Dunia bado iko nje ya mstari wa kutimiza lengo la mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi wa kuhakikisha nyuzi joto inasalia 1.5  katika kipimo cha Selsiyasi.” 

Saruji ya ujenzi wa majengo nayo inachangia katika uchafuzi wa hewa ya ukaa kutokana na jinsi ambavyo inazalishwa.
© UN-Habitat /Julius Mwelu
Saruji ya ujenzi wa majengo nayo inachangia katika uchafuzi wa hewa ya ukaa kutokana na jinsi ambavyo inazalishwa.

Amesisitiza kwamba “Ndio sababu tunahitaji matamanio zaidi katika kukakabiliana, kuhimili na kufadhili juhudi za kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Muungano wa kutokomeza kabisa hewa ukaa unatakiwa kukua zaidi na hilo ndilo lengo la Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu. Mchakato wa kuhakikisha hatuzalishi kabisa hewa ukaa unapaswa kuwa ndio kawaida kwa kila mtu, kila mhali, kila nchi, kampuni, mji, taasisi za fedha pamoja na wadau wengine wakubwa kama sekta ya usafiri wa anga , usafirishaji wa meli, viwanda na kilimo. Na wakati huohuo ahadi zote za kufikia uzalishaji sufuri wa hewa ukaa laziwe uambatane na mipango bayana na ya kuaminika kuweza kufikia lengo hilo.” 

Maneno matupu hayavunji mfupa 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba maneno matupu hayavunji mfupa na hayatoshi , ifikapo wakati wa mkutano wa COP26 amehimiza nchi zote zinapaswa kujitokeza na malengo ya matamanio ya nchi zao ili kuainisha mchango wao katika vita hivi ambavyo ni chachu kubwa ya kutimiza malengo ya maendeleo endelevu SDGs, ifikapo mwaka 2030 na amezitaka nchi tajiri zenye uchumi mkubwa duniani nan chi wanachama wa G20 kushika usukani. 

Ameongeza kuwa hawezi kusisitiza vya kutosha umuhimu wa majadiliano katika miezi hii kabla ya mkutano wa Glasgow, kwa sababu ya janga la COVID-19 kuna uwezekano mkubwa mkutano huo uliopangwa hautafanyika ana kwa ana.  

Misitu ina mchango muhimu kwa nchi nyingi katika uwezo wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi
FAO/Rudolf Hahn
Misitu ina mchango muhimu kwa nchi nyingi katika uwezo wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi

Hivyo amesema majadiliano ya maandalizi ya COP26 yatahitaji kufanyika kwa njia ya mtandao, lakini kutokana na uwezo wa nchi na muongozo wa ubunifu wa Rais wa COP na Bi. Espinosa Katibu Mtendaji wa mkutano huo, wanachama wataweza  kuendesha shughuli katika njia jumuishi nay a uwazi. 

Bwana Guterres amesema “Hatuwezi kuruhusu janga la COVID-19 kutuzuia kufanyakazi kwa pamoja katika njia muhimu ya kuelekea mkutano wa Glasgow. Ingawa kutakuwa na changamoto ni lazima tuzihimili. Gharama ni kubwa sana endapo tutafanya vinginevyo.” 

Katibu Mkuu amesema amewaagiza maafisa wote wa Umoja wa Mataifa kote duniani kuruhusu ofisi zao na vyumba vyao vya mikutano kutumia  ili kuruhusu nchi kushiriki katika majadiliano yatakayokuwa yanafanyika kwa njia ya mtandao na kuongeza kuwa “Tutasaidia mchakato huu kwa njia yoyote itakayowezekana ili kuhakikisha mafanikio yanapatikana.” 

Nchi masikini zisaidiwe. 

Katibu Mkuu amekumbusha kwamba nchi zinazoendelea hususani za visiwa vidogo na zenye maendeleo duni ni lazima zipewe msaada zinazouhitaji kuweza kuimarisha matamanio yao ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi. 

Ameongeza kuwa sayansi na wachumi wako bayana kwamba uzalishaji wa makaa yam awe ni lazima ukomeshwe ifikapo 2030 katika nchi za OECD na ifikapo 2040 katika nchi nyingine zote. 

Pia amesema ufadhili wa makaa ya  mawe na mafuta mengine ya kisukuku ni lazima ukome na kuingia katika nishati safi na salama. 

 

Tweet URL

Na kwa nchi zilizoendelea amezikumbusha kwamba “Ni lazima zitimize ahadi zao zilizoweka Zaidi ya miaka 10 iliyopita za kukusanya dola bilioni 100 kwa mwaka kwa ajili ya ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi katika mataifa yanayoendelea. Lengo hili ni lazima litimizwe kabla ya mkutano wa COP26.” 

Mwisho amesema mafanikio ya COP26 yanamaanisha kwamba ushiriki pia wa waangalizi na makundi mengine ikiwemo NGO’s, vijana, wanawake na watu wa asili. 

“Tunahitaji kila sauti iwasilishwe mezxani, wakati kwa pamoja tukishughulikia zahma ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi, hakuna sauti yoyote na suluhu yoyote inayopaswa kuachwa nyuma. Mwaka 2021 ni mwaka muhimu katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabnianchi.”