Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatupaswi kukata tamaa, tuna nia ya kujinasua kutimiza SDGs:Guterres

Katika nchi zinazoendelea kama Rwanda, watu walio katika hatari kubwa ya kuathirika na janga la COVID-19 ndio wanaopewa kipaumbele
WHO
Katika nchi zinazoendelea kama Rwanda, watu walio katika hatari kubwa ya kuathirika na janga la COVID-19 ndio wanaopewa kipaumbele

Hatupaswi kukata tamaa, tuna nia ya kujinasua kutimiza SDGs:Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameiasa dunia kutopoteza matumaini hata kama mambo yanakwenda kombo katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDGs ili kutimiza lengo ifikapo mwaka 2030. 

Akizungumza kwenye tukio maalum la “Wakati wa SDG” lililofanyika leo mjini New York Marekani wakati viongozi wa dunia wakikusanyika kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 Antonio Guterres amesema “Dunia hivi sasa iko kwenye mtihani mkubwa kuliko wakati mwingine wowote , kuanzia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi hadi vita na mpaka janga la corona au COVID-19 ambao unafanya malengo ya maendeleo endelevu SDGs, kuwa mbali zaidi kufikiwa. Ingekuwa rahisi kukata tamaa, lakini hatupotezi matumaini, wala hatushindwi kujinasua, tuna njia ya kujikwamua endapo tutachagua kuifuata. Hiyo ndio maana ya wakati huu wa SDG kuja pamoja kuiokoa sayari yet una kila mmoja wetu.” 

Katika tukio hilo lililojumuisha viongozi wa ngazi ya juu kutoka nchi wanachama na kushajihishwa na kundi la muziki wa pop kutoka Korea Kusini BTS, Guterres ameongeza kuwa wiki mbili zilizopita alizindua ajenda ya pamoja ambayo ni mpango wa kuufufua mfumo wa ushirikiano wa kimataifa na kuisongeza karibu dunia katika ajenda hiyo ya pamoja. 

Kwani amesema “Kwa sababu kwa kujikwamua kwa pamoja ndio tutaweza kurejea kwenye msitari wa kutimiza SDGs.” 

Kikundi cha muziki cha BTS kimeshiriki kwenye mkutano wa SDGs ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Cia Pak
Kikundi cha muziki cha BTS kimeshiriki kwenye mkutano wa SDGs ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

 Mambo Matano ya kutilia maanani 

Katibu Mkuu amesisitiza kwamba kuna mambo Matano yanayohitaji hatua za haraka 

Mosi: Katibu Mkuu amesema tunahitaji kutokomeza COVID-19. Hatua zetu zimekuwa za taratibu mno na zisizo na usawa. Ninatoa wito kwa kudai kushikamana kwa ajili ya mpango wa kimataifa wa chanjo ambao unaoongeza mara mbili kiwango cha uzalishaji wa chanjo ili kuwafikia asilimia 70 ya watu duniani kwa chanjo ifikapo katikati yam waka ujao.” 

Pili: “Tunahitaji kuingia kwenye mchakato endelevu wa kujikwamua na wenye  usawa kwa wote, ili tusalie kwenye msitari wa kumaliza umaskini ifikapo 2030.”

Ameongeza kuwa hii inamaanisha kufanya uwekezaji kwa ujasiri katika mifumo inayounga mkono maendeleo ya binadamu ,kuanzia kwenye elimu na ulinzi wa jamii kwa wote, huduma za afya na ajira.  
Inamaanisha kuweka kipaumbele kwa watu dhidi ya faida, ikiwa ni pamoja na kupitia ushuru waendelevu, na kukomesha ukwepaji wa ushuru, utapeli wa pesa, na mtiririko haramu wa kifedha.  
Na inamaanisha kurekebisha mfumo wa kifedha wa kimataifa, kukabiliana na changamoto za madeni na kuhakikisha kuwa nchi zinazoendelea zinanufaika na mgawanyo wa hivi karibuni wa haki maalum za michoro. 

Tatu: Haki sawa kwa wanawake na wasichana. Hatuwezi kufikia SDG yoyote bila usawa wa kijinsia. Tunahitaji uwekezaji wenye ujasiri ili kuhakikisha kila msichana ana kiti darasani na ustadi anaohitaji kupanga mustakabali wake mwenyewe.”  
Tunahitaji kuvunja miundo yenye nguvu inayoruhusu ubaguzi, vurugu na ugumu wa kiuchumi unaowadidimiza chini karibu nusu ya nusu ya binadamu wote.  
Na tunahitaji kuhakikisha kuwa wasichana na wanawake wanakaa kwenye kila meza. Kuanzia kumbi za madaraka hadi vyumba vya biashara. 

Nne: lazima tumalize vita vilivyopigwa dhidi ya sayari yetu. Kwa maneno mengine, tujitolee kutokomeza kabisa uzalishaji wa hewa ukaa  ifikapo mwaka 2050.  
Kuitisha mipango kabambe ya hali ya hewa na bioanuwai. Kukomesha kabisa matumizi ya nishati ya makaa ya mawe baada ya 2021. 
Kukusanya dola bilioni 100 kwa mwaka kwa hatua mabadiliko ya tabianchi. Na kusaidia nchi zinazoendelea katika mabadiliko yao kuelekea uchumi unaojali mazingira, ambao ni kipaumbele cha juu kwa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi wa COP26 utakaofanyika huko Glasgow.

Na tano: tunakuhitaji. Ninyi nyote ni muhimu kwa urejesho wa ulimwengu. 
Ninakuhimiza ushirikiane na serikali zako kuweka watu mbele katika bajeti zao na mipango ya kufufua. Rafiki zangu, njia iko pale, chaguo ni letu. Heb una tusonge mbelkle kwa matumaini na kusadikika.”