Tuna hofu na mwenendo wa kesi dhidi ya Dmitriev- Wataalamu UN

3 Februari 2021

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa Urusi kuhakikisha kuwa kesi dhidi ya mtetezi wa masuala ya historia na haki za binadamu nchini humo Yuri Alexeevich Dmitriev inakuwa ya haki.

Wametoa tamko hilo wakati huu ambao kuna hofu kuwa mchakato wa kesi dhidi yake ni wa kisiasa zaidi baada ya mahakama kuagiza aache kutumia mwanasheria wake na badala yake atumie wakili aliyechaguliwa na serikali.

“Tuna hofu kubwa kuwa huu ni ukiukwaji wa haki yake ya kesi kuwa ya haki katika mchakato huu unaoendelea ambao unaonekana unalenga kumnyamazisha na kuharamisha kazi zake,” wamesema wataalamu hao.

Bwana Dmitriev amejitolea maisha yake kusaka ukweli na kufanya kumbukumbu ya waathirika wa janga la ukandamizaji enzi za Stalin miaka ya 1930, ikiwemo kusaka maeneo ambako watu hao waliuliwa na makaburi ya pamoja na pia kutaja majina ya watu waliozikwa kwenye makaburi hayo.

Wataalamu hao wamesema kinyume na harakati za kutokata tamaa za Bwana  Dmitriev za kuangazia kipindi hicho cha kiza, hakuna mamlaka zozote rasmi ambazo zimepatiwa idhini kuanzisha au kusaka ukweli wa mauaji hayo kwa maslahi ya umma.

“Idadi kubwa ya makaburi ya takribani watu milioni moja waliotoweka wakati wa janga hilo hayajawahi kufanyiwa utafiti, kuhifadhiwa au kulindwa,” wamesema wataalamu hao kupitia taarifa  yao iliyotolewa mjini Geneva ,Uswisi.

Kinyume chake, mamlaka za Urusi zimesaka kumnyamazisha kwa kushambulia uzingatiaji wake wa maadili na kazi yake jambo ambalo wataalamu hao wamesema “linazuia mamilioni ya familia ambao ndugu zao walifungwa au kutoweka, kushindwa kupata majibu ya kile kilichokumba wapendwa wao.”

Bwana Dmitriev amekuwa akikabiliwa na michakato ya kisheria tangu mwaka 2016, kesi ambazo kwa mujibu wa wataalamu hao hazina mashiko ya kisheria.

Mwezi Aprili mwaka 2018 aliachiliwa huru lakini mashtaka yake yaliibuliwa ten ana kisha mwezi Januari mwaka huu wa 2021 Mahakama Kuu uko Karelia ilikazia hukumu ya mahakama ya jiji la Petrozavodsk ya kutaka Dmitriev atumie wakili aliyeteuliwa na serikali.

Wataalamu hao wameandikia barua serikali ya Urusi kuelezea hofu yake ikiwemo mchakato mzima wa kesi dhidi ya Bwana Dmitriev na ukosefu wa uchunguzi wa wale waliotoweka wakati wa janga la Gulag.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter