Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yasikitishwa na hukumu ya kifungo dhidi ya mpinzani wa kisiasa Urusi

Mabango yenye maandiko ya kumuunga mkono Aleksei Navalyn huko London, Uingereza.
Unsplash/Liza Pooor
Mabango yenye maandiko ya kumuunga mkono Aleksei Navalyn huko London, Uingereza.

UN yasikitishwa na hukumu ya kifungo dhidi ya mpinzani wa kisiasa Urusi

Haki za binadamu

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCR, imeelezea masikitiko  yake kufuatia hukumu ya kifungo dhidi ya mpinzani wa kisiasa na mwanaharakati nchini Urusi, Aleksei Navalny.
 

Taarifa ya ofisi hiyo iliyotolewa na mjini Geneva, Uswisi siku ya Jumatano, na msemaji wa ofisi hiyo Ravina Shamdasani imesema pamoja na masikitiko hayo, “tunasihi mamlaka kuwaachia pia wafuasi wake ambao walishikiliwa wakiandamana kupinga kukamatwa kwake.”

Ofisi hiyo imesema “tuna masikitiko makubwa juu ya hukumu ya mpinzani wa kisiasa Aleksei Navalyn iliyotolewa na mahakama ya Moscow siku ya Jumanne ambapo amefungwa kwa tuhuma za kukiuka masharti ya hukumu ya kesi yake yam waka 2014 kuhusu matumizi mabaya ya fedha, kesi ambayo mahakama ya haki za binadamu ya Ulaya ilishaamua mwaka 2017 kuwa mchakato wake haukuwa wa haki.”

Kesi hadi kufungwa

Bwana Navalny alikamatwa huko Moscow siku ya Jumapili baada ya kurejea kutoka Ujerumani, ambako alikuwa anapata matibabu baada ya mwezi Agosti kuathiriwa na sumu ya zama za vita baridi inayoharibu mishipa ya fahamu.

Awali alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu na nusu jela mwaka 2014, hukumu ambayo baadaye iligeuzwa na kuwa miaka miwili na miezi minane ikijumuisha pia kipindi alichokuwa anashikiliwa ndani ya nyumba.

Mwanasiasa huyo wa upinzani aliugua wakati akiwa safarini kwenye ndege kutoka Tomsk, mji ulioko Siberia akielekea Moscow tarehe 20 mwezi Agosti mwaka 2020. Alipoteza fahamu kwa wiki mbili na hatimaye alisafirishwa kwenda Berlin kwa matibabu baada ya mamlaka za Urusi kumruhusu kusafirishwa.

Baadaye serikali ya Ujerumani iliripoti kuwa uchunguzi ulithibitisha kuwa sumu iliyompata ni ya Novichok.
Mwezi Septemba mwaka jana, shirika la kudhibiti matumizi ya silaha za nyuklia, OPCW linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa lilitoa taarifa likisema “kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa silaha za kemikali, tukio lolote la kumpatia sumu mtu kwa kutumia kemikali za kuharibu mishipa ya fahamu kinaonekana kuwa ni matumizi ya silaha za kemikali. Tuhuma kama hizo ni jambo la kutia hofu kubwa,” alisema Fernando Arias, Mkurugenzi Mkuu wa OPCW.

Watu 1,400 wamekamatwa

Maelfu ya waandamanaji nchini Urusi wamekuwa wakiandamana wiki za karibuni wakimuunga mkono Bwana Navalyn.

“Tunasihi mamlaka nchini Urusi ziwaachie mara moja wale wote waliokamatwa kwa kutekeleza haki yao ya msingi ya kuandamana na kukusanyika kwa amani,” amesema Bi. Shamdasani akiongeza kuwa, “kuna ripoti ya kwamba watu waliokamatwa wanafikia 1,400. Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa maandamano hayo yanafanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.”