Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani waliouawa CAR waagwa na kutunukiwa medali ya heshima

Medali zatolewa kwa waliopoteza maisha Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati.
MINUSCA/Leonel Grothe
Medali zatolewa kwa waliopoteza maisha Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Walinda amani waliouawa CAR waagwa na kutunukiwa medali ya heshima

Masuala ya UM

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, MINUSCA umewaaga walinda amani wake wawili ambao waliuawa katika mashambulizi wiki iliyopita.

Tukio la kuaga miili ya walinda amani hao limefanyika katika makao makuu ya walinda amani yaliyoko katika mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui na kuhudhuriwa na viongozi wa MINUSCA, wafanyakazi wengine wa Umoja wa Mataifa, wanajeshi na polisi.  

Mmoja wa walinda amani walioagwa ni kutoka Rwanda ambaye aliuawa katika eneo la PK12 Kaskazini mwa Bangui Jumatano ya wiki iliyopita wakati wa jaribio la kuuteka mji mkuu lililofanywa na umoja wa makundi ya waasi, CPC. Mlinda amani mwingine kutoka Burundi, aliuawa katika shambulizi la kushitukiza lililotekelezwa na kundi hilo hilo siku moja baada ya tukio la kwanza, katika eneo la Grimari kilomita 297 kutoka katika mji mkuu Bangui.  

Kamanda wa kikosi cha MINUSCA, Denise Brown ambaye pia ni Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Denise Brown amesema, (Nats)  "wakati nchi inaishi wakati wa kihistoria katika njia yake kuelekea utulivu na demokrasia, ni hali ya bahati mbaya ambayo inatuleta pamoja katika siku hii na inatukumbusha hatari ambazo sisi sote tunakabiliwa nazo, na hasa askari wetu waliotumwa kwenye kazi, katika jukumu letu la kudumisha amani.Wameanguka kwa ajili ya ulinzi wa raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wameanguka kwa ajili ya kupeleka misaada ya kibinadamu kote nchini wakati wote na chini ya hali zote, wameanguka kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano ya kisiasa ya amani na upatanisho, na wameanguka kuwawezesha watu wa Afrika ya Kati kudhibiti hatima yao kupitia sauti ya sanduku la kura katika utekelezaji wa majukumu yao kama raia. Ndugu zetu mashujaa wamejitolea maisha yao ili Jamhuri ya Afrika ya Kati iweze kuishi na kwamba wengine wasilazimishwe kulipa gharama kama hiyo.” 

Mkuu wa majeshi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Meja Jenerali Leopold Bruno Izamo, amewatunuku walinzi hao wa amani waliopoteza maisha, moja ya medali za juu za heshima nchini humo (“Médaille de Chevalier de l'Ordre de la reconnaissance centrafricaine”).

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mashambulio yanayofanywa na watu wanaodaiwa kuwa ni Muungano wa Wazalendo wa Mabadiliko, CPC na anawataka viongozi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR kufanya kila juhudi za kuwatambua wahusika wa mashambulio haya ili waweze kufikishwa mbele ya haki.