Takriban watu bilioni 1.9 Asia Pasifiki hawapati lishe bora-Ripoti UN 

20 Januari 2021

Athari za kiuchumi kutokana na janga la COVID-19 na kuongezeka kwa bei ya vyakula imepelekea takriban watu bilioni 2 Asia Pasifiki kutoweza kupata lishe bora imesema ripoti ya Umoja wa Mataifa, Jumatano. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka 2020 kuhusu uhakika wa chakula na lishe, maeneo masikini yameathirika vibaya, na watu kulazimika kula chakula cha bei ya chini na kilicho na ubora wa lishe uliopungua. Ripoti hiyo imetolewa kwa pamoja na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na shirika la mpango wa chakula na lile la afya duniani. 

Kwa mujibu wa ripoti, “mlipuko wa COVID-19 na ukosefu wa kazi katika maeneo mengi, pamoja na kuongezeka kwa ukosefu wa uhakika wa mifumo ya chakula na soko kumechochea katika kuongezeka kwa pengo la ukosefu wa usawa, huku familia masikini zenye kipato kidogo zikiendelea kubadili mlo na kucahgua lishe ya bei ya chini na zenye ubora uliopungua.” 

Wakati watu bilioni 1.9 Asia na Pasifiki wakishindwa kupata lishe bora, hatua zinapungua katika kuimarisha lishe, moja ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Kufikia mwaka 2019, zaidi ya watu milioni 350 katika ukanda huo walikuwa wanakadiriwa kuwa hawana lishe bora huku watoto milioni 74.5 chini ya umri wa miaka 5 ni wafupi kulingana na umri wao na watoto milioni 31.5 ni wembamba kulingana na kimo chao. 

Athari ni mbaya katika siku 1000 za kwanza za maisha

Mashirika hayo yamesema wakati lishe bora ni muhimu katika maisha yote ya mwanadamu, athari za lishe dunia ni mbaya zaidi katika siku 1000 kutoka uja uzito hadi pale mtoto anafika umri wa miaka miwili. 

“Watoto wachanga, aple wanapoanza kula chakula chao cha kwanza wakiwa na miezi sita wanamahitaji makubwa ya lishe nora ili kukua vizuri na kila mlo unachangia,” yamesema mashirika hayo. 

Mashirika hayo yametoa wito kuchukuliwe hatua ya mfumo jumuishi kwa kuleta pamoja mifumo ya maji na kujisafi, afya, ulinzi wa jamii na elimu kutatua changamoto zinazosababisha hali hii ili kufikia lishe bora kwa ajili ya akina mama na watoto wote. 

Badilisha sura ya utapiamlo 

Mashirika pia yamezungumzia mabadiliko katika taswira ya utapiamlo, kwa chakula kilichosindikwa na vyakula vya bei ya chini vinavyopatikana kwa urahisi kote bara Asia na Pasifiki. Kwa kawaida zikisindikwa na sukari au Mafuta, chakula hicho kwa kawaida hukosa vitamini na madini yanayohitajika kwa ajili ya ukuaji na yanaongeza hatari ya utipwatipwa, kisukari na magonjwa ya moyo. 

Ripoti imetoa wito kwa serikali kuwekeza katika lishe bora na usalama wa chakula kw aajili ya kuchagiza lishe bora, pamoja na kudhibiti mauzo na matangazo ya vyakula kwa walaji hususan watoto. Pia imesisitiza umuhimu wa hatua ndani ya sekta binafsi, kwa kuzingatia nafasi muhimu inayoibeba katika mfumo wa chakula na mnyororo wa thamani kwa ajili ya kufikia lishe bora. 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter