Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi waishio mijini washauriwa kula vyakula vya asili

Wakulima mkoani Kilimanjaro wakionesha mazao yao wakati wa maonesho ya siku ya chakula duniani yaliyoandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.
FAO
Wakulima mkoani Kilimanjaro wakionesha mazao yao wakati wa maonesho ya siku ya chakula duniani yaliyoandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.

Wananchi waishio mijini washauriwa kula vyakula vya asili

Afya

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la chakula na kilimo duniani, FAO na la mpango wa chakula WFP nchini Tanzania wametumia maadhimisho ya siku ya chakula duniani mwishoni mwa wiki yaliyofanyika mkoani Kilimanjaro kuwataka wananchi kuondokana na kasumba ya kupenda vyakula kutoka nje ya nchi na badala yake wazalishe na kula vyakula vya asili kama njia mojawapo ya siyo tu kuimarisha lishe bali pia mifumo ya uzalishaji chakula. 

FAO na WFP walifika eneo la Machame mkoani Kilimanjaro na kuchagiza hatua hiyo ili hatimaye vyakula vya asili kama vile viazi vikuu vikitambulika kwa lugha ya asili ya Kichaga kama Vibere viwe na nafasi yake kwenye mlo wa binadamu badala ya kukumbatia vyakula vya kigeni na vile vile kuhakikisha vyakula vya asili vinaendelea kutoka kizazi kimoja mpaka kingine na kwa undani zaidi. 
  
Devotha Songorwa wa Redio washirika wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Kids FM ambaye ameambata na FAO akiwa kijiji cha Usari, Machame mkoani Kilimanjaro amekutana na Mathias Munishi ambaye alimueleza FAO ilivyowapatia elimu ya kuendeleza kilimo cha vyakula vya asili.  
  
“Mara kwa mara tunapata semina hasa kuhusu kulima mahindi, maharage na mbogamboga. Ningeshauri ujio kama huu uje mara kwa mara kusudi tuweze kupata ushauri zaidi.” 
  
Mathias anaeleza namna wanavyoweza kudumisha mapishi ya asili licha ya utandawazi uliopo sasa 
  
“Umri wa miaka 50 kuendelea upishi wake ni tofauti na upishi wa sasa hivi, ukitembelea nyumba zao utakuta wanapika vyakula vya asili kama magimbi, ngararimo, viazi vikuu nakadhalika lakini ukiangalia kwa sasa hivi nyumba nyingi ni mkaango mtupu. Nawashauri wale wakangaji wa mjini wazingatie sana vyakula vya asili, hivi vitu vya kukaang’a kaang’a ndio vinaharibu na kuleta magonjwa kama kisukari na mengine yasiyo elewaka.” 

FAO inapigia chepuo kilimo na lishe ya vyakula asili kama kiazi hiki kikuu kutoka Kilimanjaro nchini Tanzania kiitwacho vibere kwa lugha ya kichaga, kama njia siyo tu ya kukabili njaa na utapiamlo bali pia kuwa na mifumo endelevu ya chakula.
UN/Assumpta Massoi
FAO inapigia chepuo kilimo na lishe ya vyakula asili kama kiazi hiki kikuu kutoka Kilimanjaro nchini Tanzania kiitwacho vibere kwa lugha ya kichaga, kama njia siyo tu ya kukabili njaa na utapiamlo bali pia kuwa na mifumo endelevu ya chakula.


Katika kijiji chaTela mwalimu mstaafu Anna Swai, anaeleza baadhi ya mafungu ya vyakula yanayokamilisha mlo kamili na kutoa ujumbe kwa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha.  
  
“Makundi ya chakula kuna wanga kama ugali na ndizi, protini kama nyama maharage wanapata katika ufugaji na kulima. Natoa wito kwa wamama wanaonyonyesha wazingatie taratibu na ratiba ya kliniki kwa watoto hatimaye tutaweza kuinusuru afya ya watoto wetu.” 
  
Neema Shosho ambaye ni Afisa LISHE kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani -WFP akaeleza namna ya kuendeleza vyakula vya asili kwa kuzingatia lishe Bora.  
  
"Ili tuwe na mfumo endelevu wa chakula ni muhimu sana kuelimisha jamii yetu na kuwaambia vyakula wanavyovitumia vya asili ni vyakula bora. Kuna kasumba kwamba vyakula kutoka nje ya nchi ndio vyakula bora zaidi, hiyo siyo sahihi, vyakula vyao vya asili vinatosha na vina virutubisho vyote na nibora hata ukilinganisha na hivyo vingine kutoka nje ya nchi yetu.” 
  
Shosho pia amesema wanahamasisha uzalishaji endelevu wa vyakula ambapo katika maeneo mengine wamekuta wanajamii wanapasiana mbegu za asili 
  
Dokta Nyamizi Bundala, Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini humo ameeleza sekta ya mifugo inatoa mazao muhimu kwa afya.  
 “Kama tunavyosema nyumba inajengwa kwa matofali basi mwili unajengwa na lishe bora, tunaamini kwamba ulaji wa vyakula kutoka katika makundi mbalimbali ndipo unapoweza kuinua thamani ya sahani ya mlo.”