Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwamko mkubwa kwa wananchi wa CAR kuelekea uchaguzi mkuu jumapili

Uandikishaji wa wapiga kura kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.
MINUSCA/Hervé Serefio
Uandikishaji wa wapiga kura kwenye mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Mwamko mkubwa kwa wananchi wa CAR kuelekea uchaguzi mkuu jumapili

Amani na Usalama

Wapiga kura nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, wameanza kuchukua kadi zao za mpiga kura tayari kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika jumapili hii ya tarehe 27 mwezi Desemba. 
 

Nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, harakati zikiendelea mitaani huku katika vituo vya kujiandikishia, wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwa uchaguzi mkuu jumapili wakichukua vitambulisho vyao.

Ari ni kubwa ili kumaliza mgawanyo na ghasia uliogubika taifa hilo tangu mwaka 2013.

Sambia Cyril, mkazi wa wilaya ya Ngaragba kwenye mji mkuu wa CAR, Bangui ni miongoni mwa wapiga kura wanaosubiri kwa hamu fursa ya kupiga kura.

Sambia anasema, “nina hakikisho kuwa sasa lazima nipige kura. Natambua kuwa upigaji kura utafanyika. Hili ni jambo zuri kwa nchi yetu.”

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini CAR, Denise Brown ambaye pia ni mkuu wa jumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini humo, MINUSCA ameridhishwa na maendeleo ya usajili na uchukuajiwa vitambulisho vya kupigia kura.

Bi. Brown anasema, “kwa hiyo kile tunachoshuhudia ni wananchi kuonesha ari yao ya kupiga kura tarehe 27 mwezi huu. Tayari katika kituo hiki siku mbili na nusu tangu mgao wa kadi uanze, asilimia 65 ya wapiga kura wamechukua vitambulisho vyao. Hii ni dalili njema kuwa watu wamechukua kadi zao ili kupiga kura tarehe 27. Malizeni ghasia CAR, malizeni mzozo. Wale ambao wanadhani kuwa watavuruga nchi hawapo tena.”

Vituo vya kupigia kura ni zaidi ya 3,523 nchini kote ambako wapiga kura ndiko wanachukua vitambulisho vyao vya kupigia kura. Idadi ya wapiga kura waliojiandikisha ni zaidi ya 1,858,236.

Maafisa kutoka mamlaka ya uchaguzi ya taifa, ANE, nao wapo pia kutoa msaada wowote iwe ni taarifa za uchaguzi au jambo lolote linalohitaji ufafanuzi kwa wapiga kura.

MINUSCA pamoja na kusimamia ulinzi, ilisaidia kusafirisha kwa njia ya ana na barabara vifaa vya kupigia kura nchini kote ili kuhakikisha kila aliyejiandikisha kupiga kura anatekeleza wajibu wake wa kikatiba.