Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa walaani shambulio la Galkayo, Somalia 

Picha ya Maktaba: Familia ikirejea Galkayo Somalia baada ya kuukimbia ukame katika eneo la Buale.
UN
Picha ya Maktaba: Familia ikirejea Galkayo Somalia baada ya kuukimbia ukame katika eneo la Buale.

Umoja wa Mataifa walaani shambulio la Galkayo, Somalia 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulizi lililotekelezwa jana katika uwanja Galkayo, Somalia na kusababisha majeruhi na vifo. 

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumamosi hii na Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mjini New York Marekani, ni kuwa Bwana Guterres anatuma salamu zake za pole kwa familia za walioathirika na pia anawatakia kupona haraka wale waliojeruhiwa.  

"Ana matumaini kuwa wahusika wa shambulio hili watafikishwa mahakamani." Ameeleza Stephen Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. 

Aidha taarifa imeeleza kuwa Katibu Mkuu anasisitiza kuhusu Umoja wa Mataifa kujitolea kikamilifu kusaidia watu na Serikali ya Somalia katika vita vyao dhidi ya ugaidi, msimamo mkali wa vurugu na uhalifu wa kupangwa ili kujenga nchi thabiti, yenye amani na ustawi. 

UNSOM yatoa neno 

Mamlaka ya Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNSOM, nayo kupitia taarifa iliyotolewa jana mjini Moghadishu, Somalia, imelaani vikali shambulio hilo dhidi ya watu ambao walikuwa wamekusanyika uwanjani wakimsubiri Waziri Mkuu wan chi hiyo.  

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan amesema, "kitendo hiki cha kulaumiwa ni shambulio dhidi ya watu wote na viongozi wa Galkaayo ya Kaskazini na Kusini ambao wamefanya kazi kwa bidii kudumisha amani huko katika miaka ya hivi karibuni." 

Bwana Swan ameongeza kusema kuwa Umoja wa Mataifa unawapongeza watu wa Glakayo kwa kusimama kusimama kidete, “na tunaamini kwamba vurugu kama hizo mbaya hazitawazuia wao, au Wasomali wenzao, kuendelea na njia yao ya amani, upatanisho na utulivu.” 

Kwa mujibu war ipoti, mamia ya watu walikuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Abdullahi Isse katika jiji la Galkaayo, lililoko kaskazini kati mwa mwa mkoa wa Mudug wa Somalia, kabla ya ziara iliyopangwa Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble. Maafisa wakuu wa usalama ni miongoni mwa majeruhi.