Skip to main content

Mtoto 1 kati ya 5 anahitajii msaada wa kibinadamu, UNICEF yaomba dola bilioni 2.5 za Kimarekani kusaidia. 

Mandugu ambao walipoteza kaka yao kufuatia mashambulizi ya kilipuzi wakiwa shuleni jimbo la Nangarhar.
© UNICEF/Marko Kokic
Mandugu ambao walipoteza kaka yao kufuatia mashambulizi ya kilipuzi wakiwa shuleni jimbo la Nangarhar.

Mtoto 1 kati ya 5 anahitajii msaada wa kibinadamu, UNICEF yaomba dola bilioni 2.5 za Kimarekani kusaidia. 

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limetoa ombi la juu kabisa kuwahi kuombwa na shirika hilo, dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa ufadhili wa dharura, taarifa iliyotolewa hii leo mjini Amman Jordan imeeleza.  

Fedha hizo zitatumika kushughulikia mahitaji ya watoto milioni 39 kwa msaada wa kuokoa maisha Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini mwakani yaani 2021. Hii ni pamoja na ongezeko la karibu dola milioni 500 kuendelea kushughulikia janga la COVID-19 katikati ya kuongezeka kwa maambukizi kote katika ukanda huo. 

Ted Chaiban, Mkurugenzi wa Kanda wa UNICEF Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amesema, "Kanda hii ina makao ya idadi kubwa zaidi ya watoto wenye uhitaji ulimwenguni. Hii kwa kiasi kikubwa inatokana na migogoro iliyosababishwa na wanadamu pamoja na mizozo ya kijeshi, umaskini na kudorora kwa uchumi. Ombi hili linakusudia kuwafikia watoto na msaada muhimu wa kibinadamu na kuendelea kujibu mahitaji makubwa yanayotokea kama matokeo ya janga la COVID-19.” 

UNICEF imesema ushughulikiaji wa mizozo huko Yemen, Syria na Sudan ni sehemu kubwa ya ombi hili. Miaka kumi katika vita huko Syria, mojawapo ya vita vya muda mrefu na vya kikatili katika nyakati za hivi karibuni, watoto milioni 4.8 wanahitaji msaada. Katika nchi jirani, watoto milioni 2.5 ni wakimbizi wa Syria. Nchini Yemen, watoto milioni 12 au karibu kila mtoto, katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita anahitaji msaada. Nchini Sudan, watoto milioni 5.3 wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutokana na mafuriko ambayo yanaaminika kuwa mabaya zaidi katika karne iliyopita, mabadiliko ya kisiasa na mzozo wa kiuchumi. 

“Tunahisi uchovu kufadhili mizozo ya muda mrefu kama vile Yemen na Syria. Suluhisho la mizozo hii ni kupitia mkondo wa kiasiasa kisiasa na mchakato wa kidiplomasia. Mpaka suluhisho lifikiwe, ulimwengu hauwezi kufumbia macho mahitaji ya watoto walioathiriwa na mizozo miwili ya kutisha katika historia ya hivi karibuni." Amesema Chaiban. 

Migogoro mingine imeenea katika ukanda huo katika mwaka uliopita. Nchini Lebanoni, kuanguka kwa uchumi pamoja na ongezeko la maambukizi ya COVID-19 na mlipuko wa kutisha uliotokea bandari ya Beirut mnamo mwezi Agosti ulifanya karibu watoto milioni 1.9 kutegemea msaada. 

Sehemu kubwa zaidi ya fedha zilizoombwa katika ombi la UNICEF zitakusanywa ili kusaidia elimu ya watoto. Baada ya elimu, itafuata maji, usafi wa mazingira, afya na lishe na msaada wa kisaikolojia kushughulikia afya ya akili. 

Mwaka jana, 2019, UNICEF ilipokea nusu tu ya fedha zinazohitajika. Hata hivyo, “UNICEF inawashukuru wafadhili wote ambao wamekuwa marafiki wakubwa kwa watoto kote katika ukanda tajwa kwa miaka iliyopita. Ukarimu wao umeokoa maisha ya mamilioni ikiwa ni pamoja na kupitia chanjo, matibabu ya utapiamlo na maji safi na usafi. Tunatumai kuwa wafadhili hawa na wengine wataendelea kujitolea kwa watoto wakati tunakabiliwa na ugumu zaidi na athari mbaya ya janga la COVID-19, "amehitimisha Chaiban. 

TAGS: UNICEF, COVID-19, Coronavirus, Ted Chaiban