Jaji kutoka Uganda achaguliwa tena kuendelea na wadhifa huo ICJ

Ndani mwa mahakama ya kimataifa ya ICJ
UN Photo/ICJ-CIJ/Frank van Beek
Ndani mwa mahakama ya kimataifa ya ICJ

Jaji kutoka Uganda achaguliwa tena kuendelea na wadhifa huo ICJ

Masuala ya UM

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamechagua wajumbe wapya watano wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, iliyo chini ya Umoja huo.
 

Upigaji kura ulifanyika mara mbili jijini New York, Marekani ambapo Rais wa Baraza Kuu, Volkan Bozkir alitangaza matokeo baada ya kupokea barua kutoka Inga Rhonda King, mwakilishi wa kudumu wa Saint Vincent na Grenadines ambaye nchi yake ndio inashikilia urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Novemba.

Bwana Bozkir akitangaza matokeo amesema, “kutokana na matokeo ya uchaguzi huru uliofanyika kwenye Baraza Kuu na Baraza la Usalama, wagombea wafuatao wamepata idadi ya kura nyingi za kutosha kutoka vyombo vyote hivyo viwili. Wajumbe hao ni Yuji Iwasawa kutoka Japan, Georg Nolte kutoka Ujerumani,  Julia Sebutinde wa Uganda, Peter Tomka wa Slovakia na Hanqin Xue kutoka China. Kwa hiyo wamechaguliwa kihalali kuwa wajumbe wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICC na watahudumu kwa kipindi cha miaka 9 kuanzia tarehe 6 mwezi Februari mwakani.”

Baadhi ya majaji wamechaguliwa kuendelea tena na wadhifa wao na miongoni mwao ni Jaji Julia Sebetunde wa Uganda ambaye amekuwa jaji wa ICJ tangu mwezi Februari mwaka 2012 na kipindi kilikuwa kinaisha mwakani ndio akagombea tena nafasi hiyo.

Mwanachama hawakilishi nchi

Punde tu baada ya kuchaguliwa, mwanachama wa mahakama si mjumbe au mwakilishi wa serikali au nchi yake kwa kuwa mahakama hiyo haiundwi na wawakilishi wa serikali.

Wanachama wa mahakama ni majaji huru ambao jukumu lao la kwanza kabla ya kuanza kazi ni kula kiapo katka mahakama ya wazi kuwa watatumia mamlaka yao bila upendeleo na kimaadili.

oni mwa majaji hao waliochaguliwa baadhi yao wamechaguliwa tena kuendelea na wadhifa huo nao 

ICJ ina majaji 15 na jukumu lake ni kutatua migogoro baina ya mataifa pamoja na kupatia vyombo vya Umoja wa Mataifa ushauri na maoni kuhusu masuala ya kisheria.

Makao makuu ya ICJ ni The Hague nchini Uholanzi na ni moja ya vyombo vikuu 6 vya Umoja wa Mataifa na ni chombo pekee ambacho makao yake makuu yako nje ya jiji la New York, Marekani.

Vyombo vingine vikuu vya Umoja wa Mataifa ni Baraza Kuu, Baraza la Usalama, Baraza la Uchumi na Kijamii (ECOSOC), Baraza la Wadhamini na Sekretarieti.

Uchaguzi wa majaji wa ICJ hufanyika vipi?

Majaji wa ICJ huchaguliwa na Baraza Kuu lenye nchi zote 193 wanachama na Baraza la Usalama lenye wajumbe 15.
Wagombea wanapaswa kupata idadi kubwa zaidi ya kura katika kila chombo ambapo ni 97 kwa Baraza Kuu na 8 kwa Baraza la Usalama 

Kila baada ya miaka mitatu, nafasi 5 hubakia wazi na kuwaniwa na hakuna ukomo wa ujumbe.
Majaji wanachaguliwa kwa msingi wa sifa zao na si utaifa, lakini hakupaswi kuwepo kwa majaji wawili kutoka nchi moja kwa wakati mmoja.

Juhudi hufanyika kuhakikisha kuwa mifumo ya kimahakama ya dunia inaashiriwa ndani ya mahakama hiyo.