Iran yashinda madai yake dhidi ya Marekani huko ICJ

3 Oktoba 2018

Mahakama ya Kimataifa ya haki, ICJ huko The Hague, Uholanzi, kwa kauli moja hii leo imeamua kuwa Marekani lazima iondoe vikwazo vyake vinayozuia nchi kuiuzia Iran bidhaa hususan zile za mahitaji ya kibinadamu.

Vikwazo hivyo vya Marekani vinafuatia hatua ya mwezi Agosti mwaka huu ya nchi hiyo kujitoa kwenye mpango wa nyuklia kuhusu Iran, JCPOA, mpango ambao ulitiwa saini mwaka 2015 baina ya Iran, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi, China na Ujerumani.

Mwezi Agosti mwaka huu Iran iliwasilisha malalamiko yake mbele ya ICJ, ambacho ni chombo cha Umoja wa Mataifa, ikidai kuwa Marekani kwa kuiwekea vikwazo inakwenda kinyume na mkataba wa 1955 unaohusu ,uhusiano mwema, uhusiano wa kiuchumi pamoja na haki za ubalozi  kati yake na Marekani.

Mahakama imesema kuwa baada ya uchunguzi wake imeona kuwa baadhi ya vipengele vinavyolalamikiwa na Iran vinahusiana na maslahi ya kiusalama ya Marekani kwa mujibu wa mkataba huo wa mwaka 1955.

Hata hivyo vipengele hivyo havihusiani na uagizaji na ununuzi wa bidhaa za mahitaji ya kibinadamu na usalama wa safari za anga.

Kutokana na hali hiyo kwa hivyo, mahakama imeamua kuwa Marekani lazima iondoe vikwazo kutokana na hatua  iliyotangaza Mei 8 mwaka 2018 ili Iran iweze kuuziwa vifaa vya matibabu kama vile dawa, chakula, bidhaa za kilimo, vipuri pamoja na huduma zinaoambatana  kama vile huduma za ukarabati na ukaguzi ambazo ni muhimu hasa  kwa usalama wa safari za anga.

Uamuzi huo unaongeza kuwa, “ Marekani itahakikisha kuwa leseni zote pamoja na  vibali vinavyohitajika vinatolewa na kwamba malipo au uhamishaji wowote wa fedha za malipo kwa ajili ya bidhaa na huduma unafanyika bila vikwazo.”

Mahakamya ICJ imesema kuwa pande zote mbili lazima zijizuie dhidi ya hatua yoyote ambayo inaweza kuhatarisha  zaidi mvutano huo ulio mahakamani au kufanya usuluhishi  kuwa mgumu zaidi.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter