Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima viongozi Kigoma waelimika juu ya kilimo hifadhi 

Mkufunzi kutoka Gatsby Tanzania Finias Rafael, akionesha wakulima viongozi mbinu za kilimo hifadhi wakati wa mafunzo kwa vitendo kwenye mkoa wa Kigoma, magharibi mwa Tanzania.
FAO Tanzania
Mkufunzi kutoka Gatsby Tanzania Finias Rafael, akionesha wakulima viongozi mbinu za kilimo hifadhi wakati wa mafunzo kwa vitendo kwenye mkoa wa Kigoma, magharibi mwa Tanzania.

Wakulima viongozi Kigoma waelimika juu ya kilimo hifadhi 

Tabianchi na mazingira

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa –FAO- nchini Tanzania, chini ya programu ya pamoja ya Kigoma au Kigoma Joint Program, KJP wameendesha mafunzo ya kilimo hifadhi kwa wakulima mkoani Kigoma.

Mkoani Kigoma nchini Tanzania katika wilaya ya Kibondo, mafunzo kwa vitendo yakiendelea kwa wakulima viongozi juu ya kilimo hifadhi ambacho kinalenga kutosumbua udongo, siyo tu wakati wa palizi ya shamba, bali pia wakati wa upanzi. 

Kilimo hiki hutoa fursa ya kuchimba shimo pale tu ambapo mbegu inapandwa kwa kutumia jembe maalum au lile likokotwalo na ng’ombe, na hata magugu kuepushwa kuota kwa kupulizia dawa ya kuyaangamiza. 

Jumla ya wakulima viongozi 120 wamepata mafunzo haya kupitia shamba darasa, yakijumuisha mafunzo ya nadharia na vitendo katika kuandaa shamba, uhakiki wa mashimo, uwekaji wa mbolea ikiwemo samadi na mbolea za viwandani, upandaji wa mbegu na mbinu za kudhibiti magugu na visumbufu vya mazao shambani.  

Mkufunzi Finias Rafael alitumia hata lugha ya Kiha kutoa mafunzo na maswali yalipoulizwa wakati wa mafunzo haya ya siku tatu, majibu yalipatikana… 

Mnufaika wa mafunzo ya kilimo hifadhi yaliyoendeshwa na FAO Tanzania kwenye mkoa wa Kigoma.
FAO Tanzania
Mnufaika wa mafunzo ya kilimo hifadhi yaliyoendeshwa na FAO Tanzania kwenye mkoa wa Kigoma.

Mnufaika akafunguka.. "kilimo hifadhi ni kilimo kisichosumbua udongo, faida yake unalima shamba ndogo mavuno mengi. Manufaa kwangu kwanzia kwangu hadi kizazi chote kitakachofuata."

 FAO inasema matarajio ya baadaye ni wakulima hawa viongozi kuendesha mafunzo kupitia mashamba darasa ya kata katika vikundi vyao, na mradi utawapatia pembejeo kwa ajili ya mafunzo kupitia mashamba darasa.  

Mafunzo hayo yamefanyika katika halmashauri za Kakonko, Kibondo, na Kasulu Vijijini na Mji na kuendeshwa kwa pamoja na Mkufunzi ambaye ni mnufaika wa mafunzo ya Kilimo hifadhi kupitia shirika la GATSBY Africa.