Pande kinzani Libya zaridhia mkataba wa kihistoria, UN yapongeza

23 Oktoba 2020

Hatimaye pande kinzani nchini Libya leo hii zimepitisha makubaliano ya kihistoriaya kusitisha mapigano, hatua ambayo imepigiwa chepuo na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNSMIL ulioongoza usuluhishi,  ukisema kuwa ni kitendo cha kijasiri kinachoweza kufanikisha mustakabali salama,  bora na wenye amani zaidi kwa wananchi wa Libya.
 

Mkuu wa UNSMIL ambaye pia ni Kaimu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams ametoa pongezi hizo mjini Geneva, Uswisi hii leo wakati akizungumza na waandishi wa habari akisema, “mmekutana kwa maslahi ya Libya, kwa maslahi ya wananchi wa Libya ili kuchukua hatua thabiti za kumaliza machungu.”

Libya imekuwa katika mgawanyiko na mapigano tangu kupinduliwa kwa kiongozi wa taifa hilo Muammar Gaddaf mwaka 201. Wafuasi wa serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli wamekuwa wamezingirwa kwa miezi kadhaa, kufuatia mashambulizi kutoka majeshi ya uongozi pinzani yanayoongozwa na kikosi cha Libya National Army, LNA cha Kamanda Khalifa Haftar.

Usuluhishi unaoongozwa na Umoja wa Mataifa wa kamisheni ya pamoja ya kijeshi ikiwakilisha pande mbili, leo umefanikisha makubaliano hayo ambayo Bi. Williams amesema yataleta matumaini kwa wananchi wa Libya.

“Napongeza fikra ya uwajibikaji na azma yenu ya kurejesha umoja Libya na kusisitiza umuhimu wa kujitawala,” amesema mkuu huyo wa UNSMIL.

Matumaini ya sitisho la kudumu la mapigano

Ameongeza kuwa pande zote mbili zimekuja pamoja kwa mara ya kwanza kabisa kama walibya,, “safari ilikuwa ndefu na ngumu, lakini uzalengo wenu umewaongoza nyakati zote, na mmefanikiwa kukamilisha makubaliano kwa mkataba wenye mafanikio na wa kudumu wa kusitisha mapigano.”

Bi. Williams amesema ni matumaini yake kuwa mkataba huo utachangia katka kumaliza machungu ya walibya na kuwezesha wakimbizi walio ndani na nje ya nchi hiyo kurejea nyumbani na kwenye makazi yao na kuishi kwa amani na usalama.

UN / Violaine Martin
Kaimu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN nchini Libya Stephanie Williams akiongozi awamu ya nne ya kikao cha 5+5 cha kamisheni ya pamoja ya kijeshi nchini Libya, huko Geneva, Uswisi tarehe 19 Oktoba 2020

Kwa mujibu wake, mkataba huo unawakilisha hatua ya kipekee kwa Libya na wananchi wake. “Natumai kuwa vizazi vijavyo vya Libya vitafurahia mkataba wa leo kwa kuwa unawakilisha hatua ya kwanza ya kijasiri na kiuamuzi kuelekea suluhisho la kina la mzozo wa Libya.”

Kazi inayosubiriwa

Bi. Williams amesema bado kuna kazi kubwa imesalia katika siku na wiki zijazo za kutekeleza ahadi zilizomo kwenye mkataba huo akiongoza, “ni muhimu kuendelea na mashauriano ya kimkakati haraka iwezekanavyo ili kupunguza machungu ambayo mzozo huu umesababisha kwa wananchi wa Libya. Nafahamu kuwa wananchi wa Libya wanaweza kuwategemea na Umoja wa Mataifa uko nanyi na wananchi wa Libya. Tutafanya kile tuwezalo kuhakikisha kuwa jamii ya kimataifa inatoa msaada wake wa dhati kwenu ninyi.”
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud