Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchaguzi Libya waahirishwa, kufanyika ndani ya siku 30

Maandishi kwenye ukuta wa jengo moja huko Benghazi nchini Libya yakipazi asauti uchaguzi na demokrasia.
UNSMIL
Maandishi kwenye ukuta wa jengo moja huko Benghazi nchini Libya yakipazi asauti uchaguzi na demokrasia.

Uchaguzi Libya waahirishwa, kufanyika ndani ya siku 30

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kufuatia kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu nchini Libya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema anatambua tangazo la jana Jumatano tarehe 22 mwezi huu wa Desemba kutoka kwa Kamisheni ya juu ya uchaguzi nchini humo ya kwamba tarehe mpya ya uchaguzi itapangwa na Baraza la Uwakilishi ili awamu ya kwanza ya uchaguzi wa Rais iweze kufanyika.

Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amewaambia waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani kuwa Katibu Mkuu “anawapongeza walibya milioni 2.8 waliokuwa wamejiandikisha kupiga kura. Ni busara kuwa utashi wa watu ukaheshimiwa. Uchaguzi wa Rais na Wabunge lazima ufanyike katika mazingira sahihi ya amani ili kumaliza mpito wa kisiasa na kuhamishia madaraka kwa taasisi zilizochaguliwa kidemokrasia.”

 Ni kwa kuzingatia hilo, Bwana Guterres anatambua mapendekezo ya Kamisheni ya Kitaifa ya uchaguzi kwa Baraza la wawakilishi na anakaribisha azma kuendelezwa kwa mchakato wa uchaguzi wa Rais na Wabunge.

Kwa mujibu wa Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams, “kamisheni ya uchaguzi imeliomba Baraza la Wawakliishi kupanga tarehe nyingine ya  awamu ya kwanza ya uchaguzi ndani ya kipindi cha siku 30 kwa mujibu wa sheria ,na wakati huo huo izingatie hatua muhimu za kushughulikia changamozo zinazokwamisha kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi.”

Bi. Williams katika taarifa yake aliyoitoa leo amesema Umoja wa Mataifa na ujumbe wake nchini Libya utaendelea kuunga mkono mchakato wa uchaguzi unaoongozwa na walibya wenyewe.

Mapema jana tarehe 22 Desemba, Kamisheni ya kitaifa ya uchaguzi nchini Libya ilitangaza kuwa licha ya maandalizi yote ya kiufundi kwa uchaguzi uliokuwa ufanyike tarehe 24 mwezi huu wa Desemba, haitaweza kukudhi mahitaji yanayotakiwa na hivyo kutangaza kuahirisha uchaguzi huku ikiomba upangwe tarehe nyingine.