Usitishaji mapigano Libya wapokelewa kwa furaha na UN 

23 Oktoba 2020

Baada ya pande zinazokinzana nchini Libya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika mkutano wake na waandishi wa habari hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, amezipongeza pande hizo ambazo kwa muda zimekuwa kwenye mzozo kwa  kufikia hatua hiyo ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini hii leo mjini Geneva Uswisi chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa.  

Bwana Guterres ameanza kwa kusema, “ninakaribisha utiwaji saini wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na pande husika za Libya hii leo mjini Geneva Uswisi chini ya udhamini wa Umoja wa Mataifa.  Hii ni hatua muhimu kuelekea amani na utulivu nchini Libya. Ninazipongeza pande zote kwa kuweka maslahi ya nchi yao mbele ya tofauti zao.” 

Aidha Katibu Mkuu Guterres amempongeza Stephanie Williams ambaye ni Kaimu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams na ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNSMIL, ambaye aliongozana na pande kinzania katika juhudi za kufikia makubaliano ya leo. 

“Watu wengi sana wameteseka kwa muda mrefu sana. Wanaume wengi, wanawake na watoto wamekufa kutokana na mzozo huo.” Ameeleza Bwana Guterres.  

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Guterres, Makubaliano hayo yalizungumziwa ndani ya mfumo wa Tume ya pamoja ya 5+5 ya jeshi, na mazungumzo yakawezeshwa na Umoja wa Mataifa kwa msingi wa azimio la Baraza la Usalama la 2510 na 2542. Na ni matokeo ya duru nne za mazungumzo yaliyofanyika tangu Februari ya hii mwaka. 

“Kusitisha mapigano pia kunafuatia mkutano wa mapema mwezi huu ambao nilishirikiana na Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani, ambao ulisaidia kuimarisha juhudi za jamuiya ya kimataifa. Nashukuru nchi hizo zote zinaunga mkono upatanishi huu katika muktadha wa mchakato wa Berlin na katika mikutano iliyoandaliwa na nchi jirani. Natoa rai kwa wadau wote na watendaji wa ukanda kuheshimu vifungu vya makubaliano ya kusitisha vita na kuhakikisha utekelezaji wake bila kuchelewa.” Ameeleza Bwana Guterres. 

Vilevile Katibu Mkuu Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwaunga mkono watu wa Libya katika kutekeleza usitishaji mapigano na kufikia mwisho wa mgogoro ikiwa hiyo ikiwa ni pamoja na  kuhakikisha heshima kamili na isiyo na masharti kwa vikwazo vya manunuzi ya silaha vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.  

UNSMIL inafanya kufanya maandalizi ya kuanza tena mkutano wa majadiliano ya kisiasa wa Libya, ambao utatanguliwa na mfululizo wa mikutano na mashauriano ambayo yatawezesha kuanza tena kwa mazungumzo shirikishi, ya ndani ya Libya - yanayoongozwa na Libya na yanayomilikiwa na Libya. 

Kuhusu COVID-19 

Aidha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameutumia mkutano huo na wanahabari kurejelea wito wake ambao amesema amekuwa akitoa wito wa kusitisha mapigano kote duniani “ili tuelekeze nguvu zetu zote katika janga la COVID-19 na kwa ushawishi wa makubaliano ya Libya, sasa ni wakati wa kuhamasisha juhudi zote za kusaidia upatanishi unaofanyika kumaliza mizozo nchini Yemen, Afghanistan na Armenia na Azabajani - ambapo uhasama mkubwa unasababisha mateso makubwa kwa raia.” 

Bwana Guterres amehitimisha kwa kusema kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa mgogoro wowote kati ya hii na suluhisho linapaswa kuwa la kisisa.  

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud