Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 1.7 zaahidiwa kusaidia Sahel ya Kati

Mkimbizi wa ndani huko Kaya nchini Burkina Faso akiwa kwenye bustani yake aliyopatiwa bure na mwenyeji wake.
UNDP/Aurélia Rusek
Mkimbizi wa ndani huko Kaya nchini Burkina Faso akiwa kwenye bustani yake aliyopatiwa bure na mwenyeji wake.

Dola bilioni 1.7 zaahidiwa kusaidia Sahel ya Kati

Msaada wa Kibinadamu

Takribani dola bilioni 1.7 zimechangwa zikiwa ni ahadi kwa ajili ya kunusuru eneo la Sahel ya Kati barani Afrika linalojumuisha nchi za Mali, Burkina Faso na Niger. Mapema leo matarajio yalikuwa kukusanya dola bilioni 2.4

 

Fedha zinatokana na kikako cha ngazi ya mawaziri kilichofanyika Copenhagen, nchini Denmark hii leo ambapo kiwango hicho cha fedha ni ahadi kutoka wahisani 24.

Taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho imechanganua fedha hizo kuwa dola milioni 985.3 ni kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa miezi iliyobakia ya mwaka huu wa 2020 ilhali dola milioni 704.2 ni kwa ajili ya mwaka kesho 2021 na kuendelea.

Fedha hizo zikishatolewa, zitasaidia watu milioni 10 kwa mwaka huu hadi mwakani kwa kuwapatia huduma za lishe na chakula, huduma za afya, maji, huduma za kujisafi, malazi, elimu, ulinzi na kusaidia manusura wa ukatili wa kijinsia.

Mamia ya maelfu ya watu wanaoishi nchini Burkina Faso hawana uhakika wa chakula
UNOCHA/Otto Bakano
Mamia ya maelfu ya watu wanaoishi nchini Burkina Faso hawana uhakika wa chakula

Mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao uliandaliwa kwa pamoja na Denmark, Ujerumani, Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataita ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, watu wanaoishi kwenye maeneo ya mipakani mwa Niger, Mali na Burkina Faso hivi sasa wako katika kitovu cha mapigano, umaskini na mabadiliko ya tabianchi.

Zaidi ya watu milioni 13 kwenye eneo hilo wanahitaji msaada wa kibinadamu. Halikadhalika idadi ya watu wenye njaa kupindukia imengezeka mara tatu katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kufikia watu milioni 7.4.

Takwimu zaidi zinaonesha kuwa watu milioni 1.5 ni wakimbizi wa ndani kwenye nchi zao, idadi ambayo ni ongezeko mara 20 ikiliganishwa na miaka miwili iliyopita.

OCHA inasema kuwa zuio la kutotembea kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 pamoja na sababu nyingine, vimetumbukiza watu wengine milioni 6 kwenye umaskini uliokithiri.