Chonde chonde saidieni ukanda wa Sahel kwani umesambaratika – Baaba Maal 

20 Oktoba 2020

Wakati mkutano wa kusaka fedha kwa ajili ya Sahel ya Kati unafanyika huko Denmark hii leo, mwanamuziki mashuhuri kutoka Senegal na muungaji mkono wa shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, Baaba Mal ameandika barua ya wazi kuhusu madhila yanayokumba eneo hilo. 

“Nyumbani kwangu, Sahel, kumechutama! Kumeporomoshwa na mapigano, njaa na magonjwa. Naitwa Sauti ya Sahel. Kwa miaka kadhaa, sauti yangu imelisha mashairi na muziki wangu. Sasa napaza sauti kutoa wito kwa dunia kukomesha machungu na maumivu yanayotikisa eneo hilo zuri,” amesema Baaba kwenye barua hiyo ambayo imechapishwa kwenye gazeti moja la Kifaransa. 

Amekumbusha kuwa mamilioni wamekimbia makazi yao, wanawake na watoto wa kike wanabakwa, wazazi wanauawa mbele ya watoto wao, shule zinashambuliwa na kufungwa, vituo vya afya vimeteketezwa kwa moto. 

Kinachomsikitisha ni kwamba vilio vya wakazi wa Sahel zaidi ya milioni 2.7 waliofurumushwa makwao havisikilizwi. 

“Hili si janga la idadi tu ya watu. Nyumba ya pazia la idadi hiyo ni binadamu. Hili ni janga la ukimya na linafanyika huku milango imefungwa. Milango ya kutojali ya kimataifa ambako vilio na machozi ya watu si kitu na havisikilizwi. Hii lazima ikome!,” 

 Mwanamuziki huyo amesema yeye akiwa muungaji mkono wa UNHCR na mtu ambaye pia ameshuhudia ukubwa wa janga la wakimbizi Sahel anasihi jamii ya kimataifa ifungue macho na kutazama kile kinachoendelea. 

“Leo hii serikali duniani kote zinakutana Copenhagen kuchagiza amani, hatua na usaidizi wa kifedha kwa Sahel. Wakati mashirika kama UNHCR yanahaha kukidhi mahitaji ya jamii iliyofurumushwa makwao, lazima tutoe wito wa kukomesha ghasia ambayo imefurusha mamilioni kutoka makwao,” amesema Baaba. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud