Vita na janga la COVID-19 vyawaweka watoto katika hali mbaya Sahel:UNICEF

16 Oktoba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limesema vita vya silaha na athari za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na janga la corona au COVID-19 vimefanya hali ya Watoto kuwa mbaya zaidi katika ukanda wa Sahel.

Kwa mujibi wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis, “Watoto milioni 7.2 nchini Burkina Faso, Mali na Niger sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu ikiwa ni ongezeko la theluthi mbili ndani ya mwaka mmoja. 

Zaidi ya Watoto milioni moja kati ya hao wamelazimika kukimbia makwao na kutawanywa, huku huduma muhimu kama maji salama kwa ajili ya kuwawezesha Watoto hao kuishi  na kuzuia kusambaa kwa gonjwa la COVID-19  sasa ni adimu hususani miongoni mwa watu waliotawanywa.” 

Taarifa hiyo imesema makadirio ya idadi ya Watoto wataugua utapiamlo mwaka huu yameongezeka kwa asilimia 5. Hali imeelezwa kuwa mbaya zaidi hasa katika baadhi ya majimbo ya Burkina Faso ambayo yanahifadhi wakimbizi na wakimbizi wa ndani .  

Na katika jamii za Djibo, Gorgadji na Barsalogho idadi ya vifo miongoni mwa Watoto tayari imeshapita kiwango cha hatari. UNICEF inasema “katika nchi hizo tatu mashambulizi ya kulenga yamesababishwa kufungwa kwa shule zaidi ya 4000 kabla ya janga la COVID-19 kufunga zilizosalia. Pia kumekuwa na uthibitisho wa ukiukwaji mkubwa wa haki za Watoto ikiwemo kuwaingiza vitani kwenye mapigano, ubakaji na ukatili wa kingono pia umeongezeka kwa akiasi kikubwa hususan Mali.” 

UNICEF imesisitiza kuwa ili Sahel ya Kati iweze kujikwamua kutokana na migogo hii basi lazima nchi hizo zihakikishe kwamba Watoto wa kizazi hili wanaweza kupindua ukurasa wa machafuko na umasikini uliokithiri, lakioni kwa sasa ukanda huo unahitaji msaada ili kuhakikisha vifo zaidi haviendelei na hali haigeuki kuwa janga kubwa la kibinadamu. 

UNICEF ikishirikiana na wadau wanajitahidi kuwamikia mamilioni ya Watoto kwa misaada ya kuokoa maisha, chakula, chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali na fursa za kupata maji safi na usafi. 

Hata hivyo shirika hilo linasema changamoto kubwa ni fedha kwani hadi sasa limepokea asilimia 31 tu yad ola milioni 210 inazohitaji kwa ajili ya kutoa msaada wa kibinadamu kwa mwaka huu kwenye ukanda wa Sahel. 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud